Na Mwandishi
wetu,
Songea.
IDARA ya
uhamiaji mkoa wa Ruvuma, imewaonya watu wasiokuwa raia wa
Tanzania kutojihusisha kwa namna yoyote ile katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa
kufanyika Oktoba 25 mwaka huu, na endapo watafanya hivyo watakuwa wamekiuka
sheria za nchi.
Mbali na hilo
imeelezwa kuwa kushiriki katika uchaguzi huo kwa mtu asiyekuwa raia wa
Tanzania, kunaweza kusababisha taifa kupata viongozi wabovu wasiokuwa na
uchungu wa kuleta maendeleo kwa Watanzania.
Ofisa uhamiaji wa
mkoa huo, Hilgaty Shauri alitoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na vyombo
mbalimbali vya habari mjini songea.
Shauri aliwataka
wananchi hasa kwa wale wanaoishi maeneo ya mipakani, kutoa ushirikiano wa kutosha
kwa maafisa uhamiaji waliopo kwenye maeneo hayo, ili kudhibiti wahamiaji
haramu wanaoweza kuingia hapa nchini, na kushiriki katika zoezi la uchaguzi
huo siku ya upigaji kura.
Alibainisha kuwa vita dhidi ya wahamiaji haramu, isiachwe ikafanywa na idara ya uhamiaji pekee, bali kila mwananchi anapaswa kushiriki kikamilifu ambapo watu hao watakapoingia hapa nchini licha ya kufanya shughuli ambazo Watanzania wenyewe wanaweza kuzifanya, lakini serikali italazimika kuwahudumia kwa kuamini kwamba ni raia wake hivyo kuibebesha mzigo mkubwa usiokuwa wa lazima.
Kutokana na hali hiyo, amewaomba pia Wenyeviti na Watendaji wa vijiji na kata kuwa na utaratibu wa kukagua maeneo yao, hatua itakayosaidia kutambua watu wao na kuwabaini watu wanaoingia kinyume cha utaratibu za nchi.
No comments:
Post a Comment