Na Muhidin Amri,
Namtumbo.
SERIKALI wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, imeziagiza idara
na taasisi za serikali wilayani humo, kuhakikisha zinawajengea uwezo watumishi
wao kwa kuwapatia nafasi ya kwenda kujiendeleza kimasomo, ili
kupunguza tatizo sugu la wataalamu wa kada mbalimbali ikiwa ni lengo la kuongeza
ufanisi mahali pa kazi.
Mbali na hilo, wakuu wa idara husika wametakiwa kuwasimamia
na kufuatilia kwa karibu watumishi wazembe ambao wanafanya kazi zao kwa mazoea,
kitendo ambacho kinasababisha kutokea
malalamiko ya hapa na pale kutoka kwa wananchi.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa wilaya hiyo, Chande Nalicho
alipokuwa akizungumza na wakuu wake wa idara katika Halmashauri hiyo na kukemea
tabia ya baadhi ya watumishi, kukwamisha kwa makusudi mipango mbalimbali ya
maendeleo inayotekelezwa na serikali kwa manufaa ya jamii.
Wilaya ya Namtumbo, inakabiliwa na
upungufu mkubwa wa wataalamu katika kada mbalimbali.
“Ninawaagiza wakuu wote wa idara, hakikisheni mnatoa nafasi
kwa watumishi wenu kwenda kusoma ili kuwaongezea ujuzi na utaalamu, ambao utasaidia
kuleta tija katika wilaya yetu”, alisema Nalicho.
Alisema kuwa, elimu kwa mtumishi wa umma ni jambo muhimu na
ndiyo itakayomfanya kujiamini na kutekeleza majukumu yake kikamilifu, badala ya
kuendelea kufanya kazi kwa mazoea jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo
husika katika jamii.
Katika hatua nyingine, Nalicho amewataka wananchi wa wilaya
ya Namtumbo, kuendeleza tunu ya amani iliyopo sasa hasa kipindi hiki cha
kuelekea uchaguzi mkuu, ikiwa ni lengo la kujiepusha na vitendo vinavyoweza
kuwagawa wananchi na kusababisha nchi, kuingia katika machafuko.
Kadhalika Mkurugenzi huyo amewaomba wazee wa wilaya hiyo, kuwaelekeza
vijana wao kuhusu athari na madhara ya migogoro ya kisiasa ambayo tayari
imeshaanza kujionesha katika baadhi ya maeneo hapa nchini.
No comments:
Post a Comment