Na Muhidin Amri,
Ruvuma.
WALIMU nchini
wametakiwa kukataa kugeuzwa wapiga debe na kuwa madalali wa vyama
vya siasa, badala yake wazingatie majukumu yao ya kazi kwa kuongeza
juhudi ya ufundishaji watoto darasani, hatua ambayo itasaidia kuwaongezea uelewa
wanafunzi na kukuza taaluma hapa nchini.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi ngaga alisema hayo, mwishoni mwa wiki alipokuwa akifungua kikao cha siku tatu kwa wakuu wa shule za sekondari kutoka mikoa mitatu ya nyanda za juu kusini Ruvuma, Njombe na Iringa kilichofanyika kwenye ukumbi wa Kanisa katoliki uliopo mjini hapa.
Mbali na hilo, pia amewaonya walimu hao kutotumia maeneo ya shule kufanyia kampeni wanasiasa kwa sababu maeneo hayo, sio rasmi kwa ajili ya shughuli hizo huku akisisitiza kwamba tabia hiyo inawanyima fursa watoto, kupata haki yao ya msingi.
Ngaga alieleza
kuwa serikali haikatazi mwalimu kuwa na mapenzi na chama au mgombea
fulani, lakini hilo lifanyike mara atakapotoka shule baada ya kutimiza majukumu
yake ya kazi.
Mkuu huyo wa
wilaya ya Mbinga, alifafanua kuwa serikali haitasita kumchukulia hatua mwalimu
yeyote atakayebainika kuwa ni mtovu wa nidhamu, kutokana na kuingia katika
siasa na kuacha majukumu yake ya msingi aliyopewa na serikali kwa ajili ya
kutumikia wananchi.
Aidha amewaagiza
wakuu wa shule hizo, kwa kushirikiana na kamati zao za shule
kwenye maeneo yao kuhakikisha wanawabana wazazi na walezi, ambao
wamekuwa kikwazo kwa kutopeleka watoto wao shule ili kuweza kupunguza tatizo
sugu la utoro shuleni.
Ngaga alisema baadhi
ya shule zina idadi ndogo ya wanafunzi wanaoendelea na masomo, tofauti na idadi
halisi ya walioandikishwa kuripoti shuleni huku akisisitiza kuwa muda umefika sasa, kwa walimu na kamati zao za shule kuwasaka
watoto hao waliokacha kwenda shule ili waweze kuendelea na masomo.
Aliongeza kuwa kama
kutakuwa na mahudhurio mazuri, kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, hata
ufaulu wake huongezeka.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Umoja wa Wakuu wa shule za Sekondari (TAHOSA) Ponsian Ngunguvu, alisema
lengo la kikao hicho ni kubadilishana uzoefu hasa katika mambo ya utawala, tatizo
la migogoro kazini na kuziunganisha shule zote za sekondari kuwa kitu kimoja,
ili kuweza kupanga mikakati ya pamoja katika kuinua kiwango cha taaluma kwa
shule husika.
Ngunguvu alibainisha kuwa kufuatia kuwepo kwa umoja huo, tayari wamepata mafanikio makubwa ikiwemo kuwa na mitihani ya pamoja, katikati na mwisho wa muhula na kuboresha mazingira ya shule zao.
Hata hivyo bado
wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa rasilimali fedha, miongozo ya umoja wa
michezo kwa shule za sekondari umiseta na kukosekana kwa hatimiliki kwa shule
nyingi, jambo ambalo linasababisha migogoro ya mara kwa mara katika
jamii.
No comments:
Post a Comment