Na Steven
Augustino,
Tunduru.
BARAZA la
Waislamu Tanzania (BAKWATA) wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, limepiga marufuku vitendo
vya kufungisha ndoa juu ya dhehebu hilo, pasipo kuzingatia maadili ya dini
hiyo.
Sambamba na
kutolewa kwa tamko la baraza hilo, pia limeahidi kufuatilia kwa karibu utendaji
kazi wa viongozi wake wa dini ambao wamepewa mamlaka ya kufungisha ndoa
wilayani humo, na kwa yule atakayekiuka atachukuliwa hatua husika ikiwemo
kuzuiwa kufungisha ndoa kwa muumini wa dhehebu hilo.
Tamko hilo
lilitolewa na Shekh Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Alhaji Chilakwechi wakati
alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu, katika mahojiano maalumu yaliyofanyika
ofisini kwake katika Msikiti wa Ijumaa uliopo mjini hapa.
Kwa mujibu wa Shekh
Chilakwechi, alieleza kuwa maadili ambayo yamekuwa yakikiukwa na viongozi
wenzake wa dini hiyo, wengi wao wamefungisha ndoa ambazo zimehusisha ngoma huku
watu wakikesha na muziki mpaka asubuhi jambo ambalo ni kinyume na taratibu za
miongozo ya dini hiyo.
Alisema tayari
viongozi wenzake wa dini ya kiislamu wilayami humo, tayari wamepewa misingi,
taratibu na miongozo kwa kuwataka kutofanya hivyo, ambayo yametolewa na
Halmashauri ya baraza hilo baada ya kubaini uwepo wa ukiukwaji mkubwa ambao unafanywa
na baadhi ya viongozi wake.
Pamoja na mambo
mengine, akizungumzia juu ya suala la uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika
Oktoba 25 mwaka huu, Shekh Chilakwechi aliwataka waumini wa dini ya Kiislaamu
kutojiingiza katika malumbano ambayo yanaweza kulisambaratisha taifa letu na
kuliweka mahali pabaya.
Hata hivyo
alihimiza na kuitaka jamii hapa nchini, kudumisha tunu ya amani na utulivu
ambavyo tumerithi toka kwa waasisi wa taifa letu na kuwataka kutambua kuwa
baada ya uchaguzi huo, kuna maisha ya Watanzania ambayo yanaendelea kama vile
walivyozoea kuishi kila siku.
No comments:
Post a Comment