Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MAGARI mawili yaliyokuwa katika msafara wa kampeni wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) katika kijiji cha Mtua, kata ya Mpepai wilayani Mbinga mkoa
wa Ruvuma yameharibiwa vibaya baada ya watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Chama
Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuvamia msafara huo, na kurusha mawe huku
watu waliokuwemo ndani ya magari hayo nao wakinusurika kuumia vibaya.
Tukio hilo lilitokea Septemba 19 mwaka huu majira ya jioni,
ambapo Katibu wa CCM wilaya ya Mbinga, Zainabu Chinowa ndiye aliyekuwa
akiongoza msafara wa kampeni wa chama hicho katika kata ya Mpepai na vijiji
vyake kwa lengo la kumnadi mgombea wa nafasi ya udiwani kupitia tiketi ya chama
hicho, Benedict Ngwenya.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Chinowa alisema kuwa
wakati wakiwa barabarani wanarudi wakitokea katika kijiji cha Mtua ghafla
waliona magogo makubwa ya miti yakiwa yamewekwa barabarani, ili kuzuia wasiweze
kupita na baadaye walipojaribu kuyatoa ndipo kundi la vijana lilijitokeza na
kuanza kuwarushia mawe, ambayo yaliweza kuharibu na kuvunja vioo vya magari hayo
yaliyokuwa katika msafara huo.
“Kwa kweli tumenusurika kuumizwa vibaya, gari letu la chama
limevunjwa kioo cha ubavuni na gari lingine moja ambalo ni la mgombea wetu nalo
limevunjwa vunjwa karibu vioo vyote, tumeripoti Polisi ili hatua ziweze
kuchukuliwa”, alisema Chinowa.
Chinowa alieleza kuwa waliohusika katika tukio hilo, ni
wafuasi wa CHADEMA ambapo wakati wanafanya unyama huo, wengine walionekana
wakiwa wamevalia sare za chama hicho.
Mwandishi wa mtandao huu, ameshuhudia magari hayo yakiwa kituo
cha Polisi wilaya ya Mbinga, ambapo gari la CCM wilaya lenye namba za usajili T
545 BEW aina ya Landcruiser Hardtop limevunjwa kioo cha ubavuni upande wa
kushoto na lingine aina ya Landrover Discover, lenye namba T 797 AEN nalo
limevunjwa vunjwa vioo kwa mawe hayo ambayo yalikuwa yakirushwa.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Revocatus Malimi
alipohojiwa na waandishi wa habari alisema kuwa taarifa kamili bado
hazijamfikia ofisini kwake na kwamba, anaendelea kufanya mawasiliano na Mkuu wa
Polisi wilaya ya Mbinga ili aweze kupata undani wa tukio hilo.
No comments:
Post a Comment