Vichanja bora vya kukaushia mihogo. |
Na Muhidin Amri,
Namtumbo.
IMEELEZWA kuwa kukosekana kwa ubunifu na maeneo ya kufanyia
biashara kwa wasindikaji wadogo, bidhaa zitokanazo na zao la muhogo wilayani
Namtumbo mkoa wa Ruvuma kunasababisha kuongezeka kwa watu maskini kutokana na
wakulima husika katika maeneo mengi ya wilaya hiyo, kukosa mbinu na utaalamu wa
kilimo cha zao hilo na kujikuta wakipoteza nguvu na muda mwingi wa kufanya kazi
hiyo.
Aidha uzalishaji usiozingatia viwango vyenye ubora nayo ni
sababu nyingine, ambayo mkulima wa zao hilo anakosa mafanikio, licha ya
jitihada na nguvu kubwa anayoitumia wakati anapozalisha zao hilo.
Mbali na hilo usindikaji umekuwa ukifanywa kwa kutumia vifaa
duni, tatizo ambalo limekuwa likichangia bidhaa zinazozalishwa kutokana na
muhogo kukosa soko la uhakika, na wakulima kuendelea kuwa masikini
ikilinganishwa na wakulima wanaozalisha mazao mengine.
Hayo yalisemwa na Mratibu wa mradi wa Muunganisho Ujasiriamali
Vijijini (MUVI) mkoani Ruvuma, Ralph Kananga alipokuwa akitoa mafunzo ya
uboreshaji wa zao la muhogo na bidhaa zake kwa wajasiriamali wadogo, kutoka
vikundi vitano vilivyomo wilayani humo.
Kananga alibainisha kuwa licha ya kazi kubwa wanayoifanya
wakulima hao, bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo zana duni,
maeneo ya kufanyia biashara na kuendelea kusindika kwa kutumia njia za
kizamani.
Baadhi ya changamoto zinachangiwa na wakulima wenyewe hujikuta
bado wanaendelea kubaki kuwa maskini wa kipato, licha ya ukweli kwamba zao la
muhogo ni kati ya mazao yenye soko kubwa hapa nchini, na ulimwengu kwa ujumla.
Aidha wakulima wameshauriwa kuongeza jitihada katika uzalishaji
wa mazao bora ya muhogo na kuahidi kuwa MUVI, itaendelea kuwaunga mkono katika
mpango wao wa kupunguza umasikini kupitia kilimo cha muhogo kwa kutoa mafunzo
na mbinu mbalimbali, ambazo zitasaidia kuinua hali zao za maisha.
Mratibu huyo alieleza kuwa mradi utaendelea kuifanya wilaya
ya Namtumbo, kutambulika kimataifa kutokana na zao hilo ambalo wadau mbalimbali
wa ndani na nje, kwenda katika wilaya hiyo kujionea na kujifunza juu ya kilimo
cha muhogo.
Kutokana umuhimu huo wakulima waliojiunga kwenye vikundi vya
ujasiriamali kutokata tamaa na hali hiyo, badala yake waongeze juhudi kutokana
na MUVI itaendelea kuwa pamoja nao kwa kutoa ushauri, kuwatafutia masoko na
kuwajengea uwezo ili waweze kufanya shughuli zao katika mazingira rafiki
yatakayowafanya waweze kunufaika nayo juu ya kilimo cha zao hilo.
Hivi sasa MUVI inafanya kazi katika mikoa mitatu ya Pwani,
Ruvuma na Mwanza ambapo katika mkoa wa Ruvuma inafanya kazi zake wilaya ya
Songea, Namtumbo na Mbinga jambo ambalo limeifanya kufanikiwa katika kuongeza
ubora wa zao hilo.
No comments:
Post a Comment