Leonidas Gama akifurahia jambo na wapiga kura wake, katika moja ya mikutano yake ya kampeni jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma. |
Songea.
MGOMBEA ubunge wa Jimbo
la Songea mjini mkoani Ruvuma, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Leonidas Gama amesema iwapo wananchi wa jimbo hilo watamchagua kuwa mbunge wao,
atahakikisha anarudisha kinu cha kusindika zao la tumbaku kikiwa kinafanya kazi
ambacho kimejengwa jimboni humo kwa miaka mingi.
Mbali na hilo, Gama
ameahidi kwa wananchi wake kwamba atakuwa mstari wa mbele kuhakikisha wakulima
wa zao la mahindi, wanapata soko la uhakika la kuuzia mazao yao ili waweze
kunufaika nalo na kuwafanya wasonge mbele kimaendeleo.
Gama ametoa ahadi hiyo
juzi, alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wake wa kampeni katika kata ya
Mshangano mjini hapa ambapo pia wanachama 20, wa Chama Cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) walirudisha kadi za chama hicho na kujiunga na chama cha
mapinduzi.
Alisema wananchi wa
wilaya ya Songea ni wakulima wazuri wa mazao ya chakula na biashara, hivyo
wanashindwa kupiga hatua mbele kutokana na kuwepo kwa mizengwe ya hapa na pale
wakati wa kuuza mazao yao, kwani wajanja wachache wamekuwa wakiibuka na kwenda
mashambani kununua mazao yao kwa bei ya chini, tofauti na bei iliyopangwa na
serikali.
Pamoja na mambo mengine,
aliwaahidi wafanyabiashara wadogo maarufu kwa jina la wamachinga, mama ntilie,
wauza mchicha na matunda kwamba wakimchagua kuwa mbunge wao atafuta ushuru
mdogo ambao umekuwa kero kubwa kwao na kuwataka askari mgambo, kuacha
kuwanyanyasa wafanyabiashara hao.
Akizungumza huku
akishangiliwa na umati mkubwa wa watu, Gama alisema kuwa wilaya hiyo ina fursa
nyingi za kiuchumi zinazoweza kufanya mapinduzi makubwa ya kimaendeleo, lakini
hilo litafanikiwa tu endapo wananchi wa jimbo hilo watatimiza adhima yao ya
kumchagua kwa kura nyingi.
No comments:
Post a Comment