Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Simon Ngaga akisisitiza jambo katika moja ya vikao vyake vya kikazi wilayani humo. |
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
WAKAZI wa mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, wametakiwa kuuweka mji
huo katika hali ya usafi wakati wote ili waweze kuepukana na magonjwa
yanayoweza kutokea hapo baadaye, kutokana na taka kuzagaa ovyo.
Aidha kwa atakayekamatwa akionekana anachangia kuufanya mji
huo uwe katika hali mbaya ya uchafu kwa kutupa taka katika maeneo ambayo sio
rasmi, wamepewa onyo kwamba watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kutozwa
faini ya shilingi 50,000 pamoja na kufikishwa Mahakamani, ili iwe fundisho kwa
wengine wenye tabia kama hiyo.
Ofisa afya wa Halmashauri ya mji wa Mbinga, Felix Matembo
alitoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na
kusisitiza kuwa halmashauri hiyo, imejiwekea mikakati kabambe ya kuhakikisha kwamba
suala hilo linapewa kipaumbele ili kuweza kuepukana na madhara yatakayoweza
kuathiri jamii.
Matembo alifafanua kuwa katika kuhakikisha utekelezaji wake
unaleta ufanisi, tayari kuna vibarua ambao wameingia mikataba ya muda na
halmashauri hiyo wanafanya kazi ya ufagizi katika maeneo ya umma, kama vile
masoko, stendi kuu ya abiria na kuzunguka barabara za mji huo.
“Hivi sasa kazi hii ya usafi tunaifanya wenyewe kwa kutumia
vibarua ambao wanashughulika katika maeneo haya ya umma, mimi kama mtaalamu wa
mambo ya usafi ninahakikisha taka zote zinatupwa kwenye maghuba na baadaye
huzolewa na kuteketezwa kwenye dampo la kuhifadhia taka lililopo eneo la zamani
la uwanja wa ndege”, alisema Matembo.
Ofisa afya huyo aliendelea kubainisha kuwa mkakati mwingine
walionao katika kufanikisha hilo, kila wiki wamekuwa wakipita mtaani kwa
kutumia gari la matangazo kuwatangazia wananchi wahakikishe wanazingatia kanuni
za usafi.
Kadhalika aliongeza kuwa kwa kila mwezi, wiki ya kwanza siku
ya Jumamosi baadhi ya viongozi wa mji huo kwa kushirikiana na wananchi wamekuwa
wakitekeleza kwa vitendo katika maeneo ya kijamii, kwa kufanya usafi ikiwa ni
lengo la kuhamasisha wananchi kuzingatia masuala hayo ya usafi.
Pamoja na mambo mengine, Matembo alisema kuwa changamoto
kubwa inayoikabili ofisi yake na kusababisha wakati mwingine washindwe kumudu
ipasavyo shughuli za usafi ni upungufu wa wataalamu, ambapo kwa sasa ofisi yake
inao wawili tu na kwamba vitendea kazi kama vile magari ya kuzolea taka nalo
limekuwa ni tatizo sugu kwao, wana gari moja tu ambalo halikidhi mahitaji
husika.
Akizungumzia kwa upande wa mfumo wa maji taka katika mji wa
Mbinga, alisema tayari serikali imeagiza gari la kunyonya maji hayo ambapo siku
chache zijazo litawasili kwa ajili ya kufanya kazi hiyo, ili halmashauri yao ya
mji iweze kuondokana na adha ya kukodi gari kutoka mbali kwa ajili ya kufanyia
shughuli hiyo.
No comments:
Post a Comment