Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.
BODI ya Kahawa Kanda ya Ruvuma ambayo makao makuu ya ofisi
yake ipo wilayani Mbinga mkoani humo, imesikitishwa na vitendo vya baadhi ya
wakulima wa zao hilo wilayani hapa, kwa kutozingatia kanuni za ubora wa kahawa,
jambo ambalo linachangia kushuka kwa uzalishaji wa zao hilo.
Aidha imekemea na kuwataka wakulima hao, kuacha tabia ya
kuanika kahawa chini jambo ambalo nalo huchangia kushuka kwa ubora wake, badala
yake wanatakiwa kuanika kwenye vichanja vyenye urefu wa mita moja kutoka
ardhini, ili isiweze kupata vumbi na thamani yake isiweze kuporomoka.
Peter Bubelwa ambaye ni Meneja wa kanda hiyo, alisema hayo
wakati alipokuwa akijibu maswali ya mwandishi wetu ambaye alitembelea ofisini
kwake, kutaka kujua maendeleo ya uzalishaji wa zao la kahawa ya wilaya ya
Mbinga ambapo ni wilaya pekee mkoani Ruvuma, inayozalisha zao hilo kwa wingi.
Bubelwa alisema kuwa hali ya ubora kimsingi hairidhishi huku
akiwataka wakulima wazingatie taratibu za uvunaji, kutayarisha kahawa kwa
wakati ikiwemo kutumia mitambo ya kisasa, hasa pale wanapokoboa kahawa mbivu
mara baada ya kuivuna shambani.
Pia alieleza kuwa wadau wengi huko vijijini wilayani humo,
wamekuwa wakisema hali ya udhibiti wa ubora kwa zao hilo imekuwa sio nzuri huku
akiitaka kamati ya ulinzi ndani ya wilaya hiyo ambayo imepewa jukumu la kusimamia
hilo kutekeleza majukumu yake ipasavyo, ili kuweza kunusuru hali hiyo isiweze
kuendelea kuwepo katika maeneo mbalimbali.
Alisema kuwa serikali imewekeza mitambo (CPU) ya kukoboa
kahawa ambayo mkulima analazimika kuitumia ili kahawa iweze kuwa na ubora,
ambapo kwa wilaya ya Mbinga kuna mitambo 155 ambayo inafanya kazi.
“Jumla ya tani 13,000 za kahawa kavu, kwa msimu huu
tunakadiria kuzivuna hapa wilayani lakini mpaka kufikia Agosti 31 mwaka huu,
tayari tani 5,490 za kahawa kavu zimekusanywa kutoka kwa mkulima shambani
tayari kwa kupelekwa kiwandani kukobolewa”, alisema Bubelwa.
Hata hivyo aliwataka wakulima waachane na tabia ya kuchakata
kahawa majumbani, kwani ubora wake umekuwa ukipungua na kuifanya ikose soko na
bei nzuri pale inapouzwa mnadani Moshi.
No comments:
Post a Comment