Leonidas Gama. |
Na Muhidin Amri,
Songea.
WAKATI kampeni zikiendelea kwa wagombea wa vyama mbalimbali
vya siasa, nafasi ya Rais, mbunge na diwani wito umetolewa kwa wananchi wa
Jimbo la Songea mkoani Ruvuma kuepuka kuchagua viongozi watoa rushwa, kwani
kufanya hivyo hakutaweza kusaidia kupata kiongozi bora atakayeweza kuwaongoza
wananchi.
Mwito huo umetolewa na mgombea ubunge wa jimbo hilo, Leonidas
Gama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu
mjini hapa.
Gama ambaye pia ni Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, amewataka
wanaccm kuungana pamoja ili kuweza kuleta ushindi wa kishindo katika uchaguzi
ujao na sio kuendeleza majungu na makundi ndani ya chama hicho, ambayo
yanahatarisha uvunjifu wa amani katika jamii hasa kipindi hiki kuelekea
uchaguzi mkuu.
“Nawaomba wanachama wenzangu wa Chama Cha Mapinduzi, tuvunje
makundi tuungane pamoja ili tuwashinde wagombea wa vyama vingine vya siasa”,
alisema Gama.
Alifafanua kuwa wananchi wanapaswa kutumia haki yao ya
kidemokrasia, kuwasikiliza wagombea wote wa vyama hivyo ili waweze kuwapima na
baadaye kufanya maamuzi sahihi, yatakayoleta ufanisi katika kumchagua kiongozi
bora na sio bora kiongozi.
Gama alieleza kuwa ni vyema wananchi wakatambua kwamba,
kumchagua kiongozi anayetoa rushwa sio njia ya kukuza demokrasia ya kweli hivyo
utoaji rushwa, madhara yake ni kuwapata viongozi wabovu na wenye uchu na
madaraka ambao hawana dhamira ya kweli, katika kuwasaidia wananchi kusukuma
mbele maendeleo yao.
Alisema kiongozi anayepatikana kwa mtindo huo, jambo la
kwanza hushibisha tumbo lake kipindi aingiapo madarakani kwa kuhakikisha
anarudisha fedha zake alizowahonga wapiga kura wakati wa kampeni, huku
akiwaacha wananchi wakiendelea kuteseka na kero zinazowakabili katika maeneo
yao.
No comments:
Post a Comment