Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WANAFUNZI wanaosoma shule ya msingi Ntunduaro iliyopo katika
kata Ruanda wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, majengo wanayotumia kusomea yapo
katika hali mbaya na huenda yakabomoka wakati wowote kutokana na kujenga nyufa
zinazosababishwa na mtetemeko mkubwa wa ulipuaji wa miamba, kwenye mgodi wa
makaa ya mawe Ngaka uliopo katika kijiji hicho.
Hali ya mazingira ya shule hiyo hivi sasa ni mbaya na kwamba husababishwa
na kuendelea kwa shughuli hizo za ulipuaji wa baruti katika miamba, jambo
ambalo huenda likaleta madhara makubwa katika jamii.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga alisema hayo alipokuwa
kwenye kikao maalumu, katika kata ya Ruanda na uongozi wa kampuni ya Tancoal
Energy ambao ndio wamiliki wa mgodi huo, wakiwemo na baadhi ya wananchi wa kata
hiyo wakijadili juu ya athari mbalimbali zitokanazo na mgodi huo.