Mtambo ukiendelea na uchimbaji wa Makaa ya mawe katika mgodi wa Ngaka, huko katika kijiji cha Ntunduaro kata Ruanda wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma. |
Na Kassian
Nyandindi,
Ruvuma.
HATUA iliyochukuliwa na Serikali kupiga
mabomu kwa ajili ya kuwatawanya wananchi waliokuwa wakiandamana kwa amani katika
kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda mkoani Ruvuma, Mbunge wa jimbo la Mbinga
Gaudence Kayombo, ameshusha lawama nzito na kusema hajafurahishwa na kitendo
hicho.
Gaudence Kayombo
amesema, nguvu iliyotumika ni kubwa na hapakuwa na sababu kwa serikali kufanya
hivyo, kutokana na wananchi wa kijiji hicho madai yao wanayoyadai ni ya msingi
na muda mrefu sasa, umepita hawajatekelezewa.
Mbunge huyo alisema
hayo alipokuwa akihojiwa na Mwandishi wa habari hizi juu ya wananchi hao
wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu, wakidai fidia zao katika eneo ambalo
waliondolewa kwa ajili ya kupisha shughuli za mgodi wa Ngaka, ambapo huchimbwa
makaa ya mawe.
”Kule imetumika nguvu
kubwa ya polisi kupiga mabomu wale wananchi, hapakuwa na sababu badala yake
serikali itoke mbele na ieleze hawa wanaodai fidia zao lini watalipwa”, alisema
Kayombo.
Alisema kuwa kuna
baadhi yao wengine hawajalipwa kabisa na wananchi karibu 400 ambao awali
walilipwa fidia zao, ilionekana fedha walizolipwa ni kidogo hivyo nao walipewa
ahadi ya kuongezewa malipo mengine, jambo ambalo hadi leo hii halijatekelezwa.
Kayombo alisisitiza
akisema ni vyema serikali itimize wajibu wake, kwa kuelimisha wananchi na sio
kutumia nguvu kubwa kwa kuwapiga mabomu ambayo yanaathiri jamii.
Alifafanua kuwa
endapo tatizo hili litaonekana kuendelea kuwa sugu, yeye kwa nafasi yake yupo
tayari kuwasaidia wananchi wa kijiji hicho kufikisha madai yao kwa Mwanasheria
na hatimaye yapelekwe Mahakamani ili haki iweze kupatikana.
“Nipo tayari
kuwasaidia hawa wananchi kwa kuwatafutia Wanasheria ambao wataweza kusimamia jambo
hili kwa umakini katika kusaidia kudai haki zao, ili ziweze kupatikana”,
alisema.
Mbunge Kayombo
alisema, Wananchi wa kijiji cha Ntunduaro wanasikitishwa pia na hali ya
mazingira ilivyokuwa mbaya kwao ambapo vumbi la barabarani, wakati wa
usafirishaji wa makaa ya mawe limekuwa likiwaathiri afya zao hivyo, wanaiomba
mamlaka husika kumshauri mmiliki wa mgodi huo kuweka mazingira katika hali
nzuri.
Pia alisema
Mwekezaji wa mgodi huo wa Ngaka alitoa ahadi ya kuwajengea miundombinu ya maji
wananchi hao, lakini utekelezaji wa ahadi hiyo haujafanyika hadi sasa ndio
maana kumekuwa na malalamiko ya hapa na pale.
“Hawa wananchi leo
hawana maji ya uhakika katika kuendeshea maisha yao, hivi hapa kweli inaingia
akilini kwa binadamu ambaye ni kiumbe hai unaweza kuishi bila kupata maji safi
na salama”,? alihoji Kayombo.
Mto Nyamabeva
uliopo katika kijiji hicho ambao ndio tegemeo kubwa, maji yake yamechafuliwa na
wawekezaji hao kutokana na vumbi la sumu ya mkaa wa mawe.
Matatizo na dhuluma
iliyopo yanasababishwa na viongozi wa serikali, huku baadhi ya wananchi
wakiteseka na kuugua magonjwa mbalimbali kutokana na kunywa maji yenye
chembechembe ya sumu ya madini ya makaa ya mawe, yanayochimbwa katika mgodi
huo.
Hata hivyo mradi
huo wa makaa ya mawe unamilikiwa na kampuni ya ubia ya Tancoal Energy, ambayo
asilimia 30 ya hisa zake zinamilikiwa na serikali kupitia shirika la maendeleo
la Taifa NDC, na asilimia 70 ya hisa zinamilikiwa na mwekezaji wa kampuni ya
Intra Energy.
No comments:
Post a Comment