Waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi, Shukuru Kawambwa. |
Na Dustan Ndunguru,
Songea.
SERIKALI mkoani Ruvuma imewataka wazazi na walezi
kuhakikisha wanafuatilia kwa ukaribu mienendo ya watoto wao, ili wasijiingize
katika vitendo viovu ambavyo vinawafanya washindwe kuendelea na masomo yao.
Mkuu wa mkoa huo Said Mwambungu alisema baadhi ya wazazi na walezi
wamekuwa na kawaida ya kutofuatilia watoto wao, jambo ambalo halipaswi
kuendelea kuvumiliwa, kutokana na ukweli kuwa madhara yake ni makubwa pale
wanapojiingiza katika matendo yasiyokubalika mbele ya jamii.
Mwambungu alisema alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi
wa habari hizi, huku akisisitiza kila mtoto anayefikisha umri wa kuanza shule
anapaswa kuandikishwa na awapo shuleni maendeleo yake yanapaswa kufuatiliwa kwa
ukaribu, kwa ushirikiano kati ya walimu na wazazi au walezi.
Alisema walio wengi wanadhani kwamba mwalimu pekee ndiye mwenye
jukumu la kufuatilia maendeleo ya mwanafunzi, wakati inafahamika wazi kuwa yeye anakuwa nao
tu pindi wawapo shuleni lakini mara wakishatoka na kwenda majumbani kwao,
wazazi ndio wanapaswa kubeba jukumu hilo.
Alisema wakati huu ambao wanafunzi waliohitimu elimu ya msingi
wanasubiri majibu yao hawana budi kuwa makini, kwani baadhi ya wazazi au walezi
wao wamekuwa na kawaida ya kutowatendea haki watoto wa kike ambapo wakati
mwingine hukimbilia kuwaozesha, kitendo ambacho kamwe hakiwezi kukubalika
katika jamii.
Mwambungu alisema watoto wa kike wanahaki sawa kama ilivyo kwa
watoto wa kiume, hivyo jitihada zifanyike ili kuhakikisha hawarubuniwi na watu
ambao hawawatakii mema na wale ambao watabainika kuendekeza vitendo hivyo, watachukuliwa
hatua za kisheria.
No comments:
Post a Comment