Na Kassian Nyandindi,
Songea.
BUSTANI Mama za kuzalishia miche ya
kahawa, wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma zipo katika hali mbaya na huenda
uzalishaji wa miche hiyo ukashindwa kuendelea, kutokana na Halmashauri ya
wilaya hiyo kuzitelekeza bustani hizo kwa kutosimamia na kufuata taratibu
husika.
Sambamba na hilo uongozi husika wa
wilaya hiyo umeshushiwa shutuma nzito juu ya uzembe huo, kwa kile kilichoelezwa
kuwa licha ya Taasisi ya Utafiti wa zao la Kahawa Tanzania (TaCRI) – Ugano
Kanda ya kusini, kutoa ushauri wa mara kwa mara juu ya kuendeleza bustani hizo
hali ambayo hivi sasa imekuwa tete na hakuna utekelezaji unaofanyika.
Meneja wa Kanda ya Kusini Godbless
Shao, alisema hayo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari mjini hapa
ambapo alitahadharisha kuwa, endapo suala hilo litaendelea kupuuzwa huenda
uchumi wa wilaya ya Mbinga ukashuka kwa kasi, kutokana na tegemeo kubwa la
kukua kwa uchumi wilayani humo hutegemea zao la kahawa.
Shao alieleza kuwa bustani hizo
ambazo zilianzishwa na TaCRI baadaye kukabidhiwa halmashauri hiyo kwa ajili ya
kusimamia na kuendeleza uzalishaji wa miche ya kahawa, hivi sasa zinaelekea
kufa kutokana na kuwepo usimamizi duni wa wataalamu husika.
“Ni jambo ambalo kwa kweli
tusipokuwa makini na tukafanyia mzaha hizi bustani kwa sasa zina hali mbaya,
baadhi yake zina kufa licha ya TaCRI kutoa mchango wake mkubwa, nina imani hapo
baadaye tusipo zingatia kanuni za uzalishaji bora wa kahawa uchumi wa wilaya
hii huenda ukashuka na hili linasikitisha sana,
“TaCRI tayari kazi kubwa tumeifanya
kwa kujenga bustani nyingi za kuzalishia miche, lakini sasa zina hali mbaya
kutokana na Halmashauri ya wilaya ya Mbinga kutoshughulikia bustani hizi”,
alisema Shao.
Hata hivyo Meneja huyo kwa upande wa
Wakulima wanaojishughulisha na uzalishaji wa kahawa wilayani humo, aliwataka
kuendelea kuzingatia kanuni bora za kilimo ikiwemo matumizi bora ya mitambo ya
kukobolea kahawa mbivu vijijini.
No comments:
Post a Comment