Washtakiwa ambao wanatuhumiwa kufanya maandamano haramu, wakiwa katika Mahakama ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wakisubiri kusomewa mashtaka yao. (Picha na Kassian Nyandindi) |
Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.
WATU saba wakazi wa
kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wamepandishwa
kizimbani katika Mahakama ya wilaya ya Mbinga mkoani humo kwa tuhuma ya kufanya
maandamano haramu, kuziba barabara na kuharibu mali.
Katika mahakama hiyo
mwendesha mashtaka msaidizi wa polisi Inspekta Nassibu Sued Kassim, alidai
mbele ya Hakimu Joackimu Mwakyolo kuwa tukio hilo lilitokea Oktoba 10 mwaka huu
majira ya saa 2 asubuhi.
Inspekta Kassim alidai
mahakamani hapo kuwa watuhumiwa hao vilevile walishambulia kibanda cha walinzi
wa kampuni ya Tancoal Energy, ambayo inafanya shughuli za uchimbaji wa makaa ya
mawe kijijini hapo na kusababisha hasara ya shilingi milioni 2.
Aliwataja washtakiwa hao
kuwa ni Siprian Mhagama, Jackson Nkwera, Ambrose Mhagama, George Nkondora,
Theodos Komba, Angelus Mgaya na Martin Mapunda.
Kesi hiyo itakuja
kutajwa tena Oktoba 24 mwaka huu na washtakiwa wamenyimwa dhamana baada ya
Mwendesha mashtaka huyo kuiomba mahakama kuwa endapo watapatiwa dhamana,
watuhumiwa hao wanaweza kuvuruga ushahidi kutokana na shauri hilo bado
linaendelea kwa uchunguzi na baadhi ya watuhumiwa wengine bado wanatafutwa na
jeshi la polisi kutokana na kutokomea kusikojulikana.
No comments:
Post a Comment