Monday, October 28, 2013

MKUU WA WILAYA YA TUNDURU APONGEZWA KWA UAMUZI WAKE WA KUINGIA DARASANI KUSHIKA CHAKI NA KUFUNDISHA


Na Steven Augustino,
Tunduru.

UMOJA  wa  Vyama vya Walimu Tanzania (CWT) Kanda ya kusini inayoihusisha mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi(UWARUMLI) umempongeza Mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho kwa uamuzi wake wa kushika chaki na kufundisha somo la Hisabati, katika shule ya sekondari  ya Mataka wilayani humo.

Pongezi hizo zilizotolewa kwenye kikao chao kilichofanyika katika ukumbi wa Klasta ya walimu mlingoti mjini Tunduru.
 
Mwenyekiti wa Mkutano huo wa CWT, mkoa wa Lindi  Mwalimu Mlami Seba  ndiye alitanguliza pongezi hizo wakati akifungua mkutano huo kwa wajumbe wa Umoja huo kanda ya Kusini ambao walikuja kuhudhuria ambapo alisema huo ni mfano wa kuigwa na ni moyo wa pekee.

Seba aliendelea kufafanua kuwa Nalicho anapaswa kutolewa mfano kutokana na  upendo aliouoonyesha kwani  wapo viongozi wengi  ambao baada ya kuchaguliwa ama kuteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali, huacha kuzifanyia kazi taaluma walizonazo ambazo wamezisomea  kwa madai ya kuwa na kazi nyingi za Kitaifa.

Kamati ya Walimu waliokwenda kutembela shule ya Mataka Sekondari  kwa lengo la kusikiliza kero mbalimbali kutoka kwa walimu wa shule hiyo  walishitushwa na kitendo cha kumkuta mkuu wa Wilaya hiyo Nalicho, akiwafundisha darasani somo la Hisabati wanafunzi wa kidato cha nne wanaotarajiwa kufanya mtihani wa mwisho wa taifa mwezi November mwaka huu.

Mkuu  wa wilaya ya Tunduru  Chande Nalicho aliahidi kuingia darasani na kuanza kufundisha somo la Hisabati, mapema mwaka huu wakati alipokuwa katika ziara yake ya kikazi wilayani humo.
  

No comments: