Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
IMEELEZWA kuwa vitendo vya uharibifu wa vyanzo vya maji
katika eneo la Mamlaka ya mji mdogo wa Mbinga mkoani Ruvuma, endapo havitadhibitiwa
mapema huenda vikashindwa kuendelea kutoa maji, kutokana na wakazi wa mji huo
kuendesha shughuli za kilimo katika vyanzo hivyo.
Aidha uharibifu huo unatokana na wakazi hao kukata miti
iliyorafiki ya maji ambayo ipo kwenye vyanzo, jambo ambalo nalo linahatarisha
kutoweka kwa uoto wa asili.
Hayo yamejitokeza katika kikao cha Baraza la Mamlaka la mji
huo, kilichoketi kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa, ambapo wajumbe
wa baraza hilo walilalamikia hali hiyo na kuutaka uongozi wa wilaya kuchukua hatua
mapema kabla ya tatizo kuwa kubwa.
“Hili suala inabidi tuliangalie kwa kina zaidi hapa wataalamu
wanaosimamia mazingira tunao hatuelewi wanafanya nini, tufute mambo ya siasa
turudishe uoto wa asili katika vyanzo vyetu ili tuweze kuepukana na tatizo
linaloweza kutokea hapo baadaye”, alisema Issack Ndunguru Mwenyekiti wa
kitongoji cha Mbuyula.
Naye Mwenyekiti wa Mamlaka hiyo Steven Matteso alisema
itakuwa si busara kuongea kwa mzaha kuhusiana na suala hilo la vyanzo vya maji,
ni vyema ushirikiano ufanyike katika hili kwa kuhakikisha vyanzo hivyo ambavyo
huzunguka mji huo vinakuwa salama.
“Nina hakika baada ya miaka kumi baadaye mji wetu utaingia
kwenye tatizo kubwa la upatikanaji wa maji, kutokana na vyanzo hivi kuendelea
kuharibiwa”, alisema.
Naye Kandidus Komba Mwenyekiti wa kitongoji cha Tugutu,
alisema ni vyema elimu itolewe kwanza kwa wananchi juu ya umuhimu wa kutunza
vyanzo vya maji na suala hili lisiishie kuzungumzwa katika vikao.
Pamoja na mambo mengine Diwani wa Kata ya Mbinga mjini,
Kelvin Mapunda alisema ni wakati sasa kwa serikali ya wilaya ya Mbinga kupanga
utaratibu wa kuzalisha miti rafiki ya maji, na kuwagawia wananchi bure kwa
ajili ya kupanda katika maeneo ambayo vyanzo vya maji vimeathiriwa.
No comments:
Post a Comment