Na Muhidin Amri,
Ruvuma.
VIJANA nchini wamehimizwa kujikita
zaidi katika shughuli za maendeleo na kujiepusha kushiriki katika mambo
yasiokuwa na manufaa kwao, ambayo yanaweza kuwaharibia mustakabali wa maisha
yao ikiwemo kushiriki kwenye maandamano ya vyama vya siasa ambayo mara
nyingi yamekuwa na dhamira ya kuanzisha chuki na uhasama, kati ya serikali na
wananchi.
Hayo yamesemwa hivi karibuni wilayani
Songea na Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Senyi Ngaga, wakati akifunga
mafunzo ya miezi mitatu kwa vijana wa kujitolea Operesheni miaka 50 ya
JKT na miaka 50 ya vijana kwa mujibu wa sheria, Julai hadi Septemba mwaka huu
katika kikosi cha 842 KJ Mlale JKT mkoani humo.
Mkuu huyo wa wilaya alisema vijana
wana nafasi kubwa ya kulifanyia mambo mazuri taifa hili, tofauti na wao
wanavyofikiria lakini inaonesha kwamba tatizo kubwa walilonalo ni kutojitambua
ndiyo maana wanadiriki kushiriki katika mambo ambayo ni tofauti na umri
walionao na hata kujikuta wakipoteza muda wao mwingi, katika vitu ambavyo vinavyowapotezea muda.
Alikemea tabia iliyoanzishwa na
baadhi ya vyama vya siasa kuwahamasisha vijana kuanzisha fujo, badala ya
kuwahimiza kushiriki katika kazi za ujenzi wa taifa hili licha ya kufahamu kuwa
vijana ndiyo taifa la kesho na hakuna nchi yeyote duniani iliyopiga hatua za kimaendeleo
bila ya mchango wa vijana wake.
Ngaga alisema tabia inayofanywa na
viongozi wa vyama hivyo haifai na inatakiwa kukemewa na kukomeshwa, lakini hayo
yote yanawezekana iwapo tu vijana wenyewe watakataa kutumiwa na watu hao
kwa masalahi yao binafsi na kusisitiza kuwa taifa lolote haliwezi kupiga hatua mbele,
kwa watu wake kushiriki maandamano au kufanya fujo.
Aliongeza kuwa lengo la Serikali
kurudisha mafunzo ya JKT ni kutaka kuwakusanya vijana kutoka sehemu mbalimbali
nchini, ili kuwafundisha uzalendo wa nchi yao na wengine watakao bahatika
kupata ajira serikalini, wawe viongozi bora watakaowasaidia watanzania wenzao
katika kujenga nchi imara na yenye mshikamano thabiti.
Alibainisha kuwa vijana wengi ambao
kwa sasa ni viongozi katika idara za serikali na hata mashirika ya umma
waliopitia mafunzo hayo wamekuwa viongozi wazuri katika taifa hili,
ukilinganisha na wale waliopata nafasi hiyo bila ya kupitia mafunzo hayo na
matokeo yake kila siku wamekuwa watu wa kulalamika badala ya kutafuta njia ya
kuwasaidia wenzao, kutafuta suluhu ya kero au matatizo yanayowakabili.
Katika mafunzo hayo
jumla ya vijana 1123 kati yao wavulana 890 na wasichana 238 walihitimu mafunzo
ya awali ya kijeshi katika kikosi hicho, ambapo pia kwa wale wa kujitolea
wataendelea na kozi za fani mbalimbali za ujasiliamali.
No comments:
Post a Comment