Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete. |
Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.
IKULU ndogo ambayo anaishi Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani
Ruvuma Senyi Ngaga, imevamiwa na watu wasiojulikana ambao wanadaiwa kuwa ni
wezi, na kuvunja banda la kufugia kuku na kuwaiba.
Uhalifu huo umetokea majira ya usiku wa Oktoba 2 mwaka huu na kuiba kuku kadhaa, ambao walikuwa wamehifadhiwa katika banda hilo ambalo limejengwa kwa tofari katika eneo la nyumba anayoishi Mkuu huyo wa wilaya.
Aidha imeelezwa kuwa wizi huo umetokea baada ya wezi hao kutoboa ukuta wa chumba ambacho kuku hao walihifadhiwa, ambapo inadaiwa kuwa askari waliokuwa lindoni hawakuwa makini katika kutimiza majukumu yao.
Chanzo kimoja cha habari kutoka jeshi la polisi wilayani Mbinga ambacho hakikutaka jina lake litajwe gazetini kilitoboa siri na kusema, askari waliokuwa zamu siku hiyo katika eneo hilo la Ikulu, walilala usingizi ndio maana wizi huo ulitokea.
“Ni tukio ambalo linatuumiza sana kichwa kwa eneo kama hili kuvamiwa na kuvunjwa, huu ni uzembe kwa askari kwenda kulala usingizi na kuacha eneo la lindo”, alisema.
Pamoja na mambo mengine wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi, baadhi ya wakazi wa mji wa Mbinga wamesema kuwa ni jambo la kushangaza kwa eneo hilo kuvamiwa na wezi, hivyo ni vyema ulinzi ukaimarishwa ili matukio kama haya yasiweze kuendelea kutokea.
“Mkuu wa wilaya ni mwakilishi wa Rais wetu inakuwaje eneo la Ikulu ndogo kama ile ambapo anaishi panavamiwa na wezi, wakati vyombo vya usalama vipo, vina fanya kazi gani”, walihoji.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma Deusdedith Nsimeki amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema, “ni kweli taarifa juu ya kuvamiwa na kuvunjwa banda la kufugia kuku katika eneo hilo nimezipata hivi punde, kuku kadhaa wameibwa idadi yake bado sijaipata lakini uchunguzi bado unaendelea ili tuweze kubaini ni nani aliyehusika na uhalifu huo, kwa hivi sasa hakuna mtu tunayemshikilia”.
No comments:
Post a Comment