Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MFANYABIASHARA mmoja ambaye ni raia
mwenye asili ya kiarabu amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya wilaya ya
Mbinga mkoani Ruvuma, kwa kosa la kutunza silaha kwa uzembe kitendo ambacho ni
hatari katika jamii.
Kwa mujibu wa Mwendesha mashataka wa
polisi Inspekta Mwamba alimtaja raia huyo kuwa ni Karama Abdallah Karama (37)
ambaye anaishi Mbinga mjini, alitenda kosa hilo Oktoba 10 mwaka huu majira ya
saa 5:30 asubuhi.
Mwendesha mashataka huyo alidai mbele
ya Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama wilaya hiyo Geofrey Mhini kuwa, silaha
hiyo ni Pisto aina ya Bereta yenye namba za usajili H 30436Y.
Alisema raia huyo alikamatwa
na maofisa wa Jeshi (JWTZ) ambao walikuwa kwenye oparesheni “Okoa Maliasili”,
ambapo walipobaini uzembe huo walimuamuru mfanyabiashara huyo aitoe silaha
ambayo ilikutwa ikiwa imehifadhiwa katika eneo la kituo cha mafuta cha Oil Com
kilichopo mjini hapa, ikiwa katika mazingira ya hatari.
Maofisa hao wa Jeshi wakati huo
walikuwa wakimfanyia upekuzi Bw. Karama, baada ya kuihisiwa anafanya biashara
ya kusafirisha Nyara za serikali pasipo kibali maalum ndipo walipobaini kuwepo
na tatizo la uzembe wa utunzaji wa silaha, ambayo anaimiliki kisheria.
Ilidaiwa Mahakamani hapo kuwa wakati
maofisa hao wa Jeshi wakiwa katika eneo hilo la tukio cha kushangaza mshtakiwa
huyo alipokuwa chini ya ulinzi huku akiambiwa aitoe silaha, yeye alikuwa
akikataa huku akimwambia mfanyakazi wake wa chini aliyekuwa katika eneo hilo la
kituo cha mafuta aitwaye Athumani Said, kwamba akaichukue ipo ndani ofisini
kwake ambapo mfanyakazi huyo alikataa na kumtaka aende akaichukue mwenyewe.
Inspekta Mwamba alisema baada ya
majibizano ya muda mrefu ndipo maofisa wa JWTZ kikosi cha Okoa Maliasili,
walichukua jukumu la kumuamuru mshtakiwa aende akaichukue yeye mwenyewe na
baadaye alitii amri na kwenda kuichukua, ndipo waliikuta ikiwa kwenye mkoba wa
plastiki katika mazingira ya hatari.
Silaha hiyo ilikutwa na risasi 23
zilizokuwa na magazine mbili ambapo mshtakiwa huyo alianza kuimiliki kisheria
mwaka 2008.
Hata hivyo kesi hiyo itakuja kwa
ajili ya kusikilizwa tena Novemba 11 mwaka huu na kwamba mshtakiwa yupo nje kwa
dhamana.
No comments:
Post a Comment