Monday, October 14, 2013

TUNDURU MISHAHARA YA WALIMU NI TATIZO

Waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi, Shukuru Kawambwa.

























Na Steven Augustino,
Tunduru.


ZAIDI ya watumishi 250 wa halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, hawajaenda kazini kwa muda wa wiki tatu sasa, wakiwa wanasubiria kupokea mishahara yao.


Hali hiyo imetokana na kuwepo kwa sintofahamu iliyodaiwa kusababishwa na ofisi za Hazina, baada ya kuwaingizia mishahara yao ya mwezi wa tisa mwaka huu huku ikiwa na nyongeza ya mapunjo ya mishahara yao ambayo inadaiwa kuwa majina ya watumishi hao hao kuwa ndio walioingiziwa fedha hizo, kupitia utaratibu huo katika mishahara yao waliyolipwa mwezi wa tisa mwaka 2012.


Wakizungumza na mtandao huu kwa nyakati tofauti baadhi ya watumishi hao pamoja na kuwatuhumu viongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo kutofuatilia na kutatua tatizo hilo, katika ufuatiliaji wa haki zao hizo walisema kuwa hali hiyo imewafanya kuishi katika maisha duni na wengine kuwa ombaomba kwa watu ili waweze kuhudumia familia zao.


Walisema kutokana na hali hiyo pia watumishi hao wakiwemo walimu wanaofanya kazi zao nje ya mji wa Tunduru, wameshindwa kurejea katika vituo vyao vya kazi kutokana na kukosa hata fedha za kujikimu wakati wanasubiri hatima ya kupatikana kwa mishahara yao  ambayo pia ingewawezesha kupata nauli ya kuwawezesha kurejea ma kwao katika vituo vyao vya kazi.


Katibu wa Chama Cha Walimu(CWT) wilayani humo Lazaro Saulo alisema kuwa hali ya mahangaiko wanayopata sasa wanachama wake, hivi sasa yameweka ofisi yake katika mazingira magumu na kumfanya ahamishie shughuli zake katika ofisi za Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo hadi tatizo hilo litakapo tatuliwa.


Alisema awamu ya kwanza wiki iliyopita ofisi yake ilipokea orodha ya Watumishi 253 kati yao wakiwemo watumishi wa idara ya elimu 195 wakiwa hawajaingiziwa mishahara yao na alipo fuatilia alielezwa kuwa tatizo hilo lingitatuliwa mwishoni mwa wiki iliyopita na walipo fuatilia mikshahara hiyomwanzoni mwa wiki hii walikuta wakiwa wameingiziwa kati ya Shilingi 5000 na 20,000 huku kukiwa na kundi kubwa la watumishi ambao bada akaunti zao ziliendelea kusoma Sifuli.


Alisema kufuatia hali hiyo alienda tena na kufanya mazungumzo na viongozi wa halmashauri hiyo, ambao waliendelea kumpiga danadana kwa kuombwa aendelee kuwasihi Wanachama wake hao, kuendelea kuwa wavumilivu wakati suala hilo linaendelea kushughulikiwa na Hazina.


Saulo aliendelea kufafanua kuwa kama kosa lilifanyika na hazina, hivyo anao uhakika kuwa tukio hilo halijatokea kwa watumishi wa Tunduru pekee hivyo hata kama wataingiziwa fedha hizo, kulingana na mishahara waliyopata mwezi wa nane mwaka huu kama wanavyoelekeza wataalamu wa halmashauri hiyo lakini kuna uhakika kuwa katika Salary slip zitakazo kuja mwezi wa 10 mwaka huu, zitaonesha kuwa fedha hizo zilichukuliwa na walengwa gani na kama kweli itabainika kuwa ziliingia kimakosa.


Akizungumzia tukio hilo Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Keneth Haule, pamoja na kukiri kuwepo kwa hali hiyo aliwataka watumishi hao kuwa wavumilivu hasa kipindi hiki kigumu kwao, na kwamba tayari suala hilo lilikuwa likishughulikiwa na ofisi yake kwa kushirikiana na hazina kwa ajili ya utatuzi.

No comments: