Sophia Simba akifurahi baada ya kushika mbogamboga, wakati alipokuwa akikagua shughuli za ujasiriamali zinazofanywa na akina mama wa UWT wilayani Mbinga. |
Sophia Simba akipokea maelezo juu ya namna ya utengenezaji wa sabuni za kufulia nguo na kuoshea vyombo, ambazo hutengenezwa na kundi la akina mama wajasiriamali kutoka UWT wilayani Mbinga. |
Na
Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WANAWAKE
wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wametakiwa kuwa makini katika kuendesha
maisha yao kwa kujishughulisha na kilimo, biashara na kujiunga na vyama vya
akiba na mikopo ili waweze kuepukana na kujiingiza kwenye anasa ambazo
zinachangia maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Sambamba
na hilo wameshauriwa kushirikiana na kuchukua hatua katika kukabiliana na
changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku kwa kufanya
kazi kwa bidii.
Rai
hiyo ilitolewa na Waziri wa Maendeleo ya jamii, Jinsia na watoto Sophia Simba
wakati alipokuwa akizungumza leo na Wanachama wa Umoja wa Wanawake Tanzania
(UWT) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kwenye uwanja wa ofisi za Chama Cha
Mapinduzi (CCM) mjini hapa.
Simba
yupo katika ziara yake ya siku mbili wilayani Mbinga, kwa lengo la kuwatembelea
wanawake wa Umoja huo na kukagua shughuli mbalimbali za ujasiriamali, ambazo
huendeshwa na akina mama hao wilayani humo.
“Ndugu
zangu sasa ni wakati wa kujituma na kufanya kazi kwa bidii, wanawake
wengi tumekuwa tukijiingiza kwenye anasa kutokana na kutokuwa na ajira kama
njia ya kujipatia kipato, yatupasa tubadilike tuachane na mambo haya”, alisema
Simba.
Alisema
huu ni wakati wa wanawake kujikwamua kiuchumi kwa kujiunga kwenye SACCOS ambazo
zitawasaidia kuwajengea uwezo kwa kupata mikopo ya kuanzisha na kuimarisha
miradi yao.
Aidha
alieleza kuwa wanawake wanapaswa kujiendeleza kielimu na kwamba huu ni wakati
wa kupambana na maisha badala ya kushindana kwa mambo yasiyo ya msingi.
Waziri huyo
pia alikemea kitendo cha akina mama kuwapiga na kunyanyasa watoto wadogo, na
kuwataka vitendo hivyo kuachana navyo.
“Naomba
mjue haki ya mtoto anapaswa kulindwa na sio kunyanyaswa, nahitaji tuwe karibu
sana na watoto wetu kwa kuwapatia malezi bora na sio kuwapiga”, alisisitiza.
Hata
hivyo aliwataka wanawake kutambua kuwa wao ni kiungo muhimu katika jamii hivyo
ni vyema serikali, ikawawekea vipaumbele mbalimbali ili waweze kujikwamua
kimaisha kwa kuwa asilimia kubwa wao ndio walezi wa familia.
No comments:
Post a Comment