Ziwa Nyasa. |
Na Dustan Ndunguru,
Nyasa.
JUMUIYA ya Umoja wa wanawake Tanzania(UWT) wilayani Nyasa mkoa wa
Ruvuma imeanza kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wanawake,
ambapo imewataka waunde vikundi ambavyo vitawasaidia kuwainua
kiuchumi na kuwaongezea pato katika familia zao.
Mwenyekiti wa jumuiya hiyo wilayani humo Grace Millinga alisema
wamechukua hatua hiyo ya kupita kuhamasisha wanawake wenzao kwa kuwapatia elimu
ya ujasiliamali, ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya chama cha Mapinduzi ya
mwaka 2010 baada ya kubaini wanawake wa wilaya hiyo bado wanaishi maisha duni
tofauti na wenzao wa wilaya nyingine mkoani humo.
Alisema pamoja na kuwapatia elimu ya ujasiriamali bado wamekuwa
wakiwataka kuunda vikundi na kubuni miradi ambayo itawasaidia kuwapatia soko la
uhakika, kwa kuuzia bidhaa zao na kuwa na akaunti benki kabla ya kusajili na
kutambulika kisheria kama moja ya njia rahisi ya kuweza kukopa fedha, kwenye
taasisi za kifedha.
Alisema kazi hiyo wameanza kwa kuifanya kwa kuanzia kwenye vijiji
vya mwambao wa ziwa Nyasa, na wamebaini wengi wao wamekosa elimu ya
ujasiriamali ambapo hujikuta wakijiingiza kwenye vitendo viovu vya
uasherati kwa lengo la kujipatia fedha, huku wakikabiliwa na uwezekano
mkubwa wa kupata magonjwa.
Mwenyekiti huyo pamoja na kuisifu wilaya hiyo ndio inaongoza kwa
wasomi wengi wakiwemo wanawake katika mkoa huo wa Ruvuma huku wengi wao wakiwa na
madaraka ya juu ya uongozi hapa nchini, lakini wameshindwa kuwasidia na
badala yake wamehamisha makazi yao na kwenda kuishi nje ya mkoa huo huku
akiwataka wazawa wa Nyasa waishio nje wakumbuke pia kuja kuwekeza wilayani
kwao.
Alisema wilaya hiyo ina fursa nyingi hasa kwa upande wa kilimo
ardhi yake inarutuba nzuri yenye mabonde ambayo inastawisha vizuri
minazi, korosho, matunda na mbogamboga za majani, lakini wamekosa wataalamu na
watu wa kuwasemea na kuwaacha wanawake wakihangaika wakati fursa za maendeleo
zipo ambazo zinaweza kuwainua kiuchumi na kuishi maisha mazuri.
Pia aliwataka watendaji wa serikali wakiwemo maofisa maendeleo ya
jamii wa wilaya hiyo, kufanyakazi kwa weledi kwa kuzingatia misingi na taratibu
husika badala ya kukaa ofisini na kusubiri taarifa kitu ambacho
kimekuwa kikidumaza maendeleo ya wanawake hasa wanaoishi vijijini ambao
hawafikiwi na viongozi mara kwa mara.
No comments:
Post a Comment