Gaudence Kayombo, Mbunge wa jimbo la Mbinga. |
Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma
limelazimika kutumia nguvu ya kuwatawanya wananchi wenye hasira kali, kwa
kuwapiga mabomu ya machozi ambao waliandamana wakidai fidia zao ambazo
hawajalipwa kwa muda mrefu katika eneo la mgodi wa makaa ya mawe Ngaka, uliopo kijiji
cha Ntunduaro kata ya Ruanda wilayani Mbinga mkoani humo.
Wananchi hao walizuia magari ya mgodi huo ambayo
yalikuwa yakibeba mkaa wa mawe, huku wakipaza sauti zao hadi walipwe kwanza
fedha zao wanazodai kwa muda mrefu ndipo kazi ya uchimbaji na usafirishaji wa
mkaa iweze kuendelea.
Kufuatia tukio hilo jeshi hilo la polisi linawashikilia
wanakijiji watano wakiwemo mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha
Ntunduwaro, afisa mtendaji wa kijiji hicho na afisa mtendaji
wa kata ya Ruanda kutokana na vurugu hizo.
Habari zilizopatikana mjini Songea ambazo
zimethibitishwa na Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Deusdedit
Nsimeki zimesema kuwa tukio hilo lilianza kutokea juzi
majira ya saa za asubuhi, ambako wananchi wa kijiji cha
Ntunduwaro walijipanga na kufunga barabara inayokwenda kwenye mgodi
huo wa makaa ya mawe ambao upo karibu na kijiji hicho.
Alisema wanakijiji hao walikuwa na lengo
la kuishinikiza serikali ili iwalipe nyongeza ya fidia ambayo
wanadai kuwa hapo awali walipunjwa wakati wanafanyiwa tathmini ya
mali zao zilizokuwepo ndani ya maeneo yaliyochukuliwa na mgodi huo
kwamba serikali ilitumia sheria ya zamani badala ya sheria
iliyopo hivi sasa ambayo inaonesha kuwa ni kubwa.
Alifafanua kuwa kundi kubwa la wananchi wakiwemo
watoto na akina mama waliokuwa wamekaa mbele lililojipanga ni
lile lililolipwa mwanzo kwa kutumia sheria ya uthamini ya
zamani ambapo wanadai kuwa wamekuwa wakiahidiwa mara kwa
mara na serikali kuwa watalipwa kiasi cha fedha cha
fidia kilichobakia lakini hadi sasa bado hawajalipwa.
Alieleza kuwa kutokana na hali hiyo wanakijiji hao
waliamua kuchukua uwamuzi wa kuzuia shughuli za magari
yanayobeba makaa ya mawe yasiingie kuchukua makaa ya mawe
wala kutoka kwenye eneo hilo la mgodi.
Kufuatia kuwepo kwa vurugu hizo zilizosababisha shughuli za
mgodi kusimama kwa siku mbili, polisi baada ya kupewa taarifa hiyo
walikwenda kwenye kijiji hicho wakiwa wameongozana na
katibu tawala wa wilaya ya Mbinga Idd Mponda ili
kujaribu kuongea na wananchi, kuwasihi waondoe kizuizi
hicho ili magari yaendelee na kazi ya kusomba makaa ya
mawe, lakini wananchi walikataa na walimweleza katibu tawala huyo
kuwa hawamuhitaji kumuona yeye pamoja na watu wengine wala
Mkuu wa wilaya hiyo kuwasikiliza wanachotaka walipwe
fedha zao wanazodai na si vinginevyo.
Aliongeza kusema kuwa mvutano huo wa mazungumzo kati
ya katibu tawala wa wilaya hiyo Mponda na wanakijiji
yalidumu kwa muda mrefu hadi juzi majira ya saa tatu usiku
polisi waliamua kulilinda eneo hilo na baadaye
walifanikiwa kuwakamata watu watano ambao wanadaiwa
kuwa ndio waliokuwa viongozi wa vurugu hizo.
Amewataja wanaoshikiliwa kuwa ni Mwenyekiti wa serikali
ya kijiji cha Ntunduwaro John Nyimbo, Matrida
Nchimbi ambaye ni Afisa mtendaji wa kata ya Rwanda, Joachim Ngaponda
ambaye ni Afisa mtendaji wa kijiji hicho, Mwenyekiti wa kamati ya
miradi ya kijiji hicho Gallusi Komba na John
Joachimu Mahai mkazi wa kijiji cha Malindindo tarafa ya Mbuji
wote wanaendlea kuhojiwa na jeshi la polisi mkoani Ruvuma.
Aidha Kamanda Nsimeki alisema pamoja na polisi
kuwashikilia viongozi hao na baadhi ya wananchi, mnamo jana (leo) majira
ya saa za asubuhi vurugu zilirejea tena
ambapo polisi walilazimika kutumia mabomu
ya machozi kuwatawanya wanakijiji hao ambao
waliendelea kuyazuia magari yaliyokuwa yamebeba makaa ya
mawe huku wananchi wakijitahidi kuyazuia
yasipite.
No comments:
Post a Comment