Rais Jakaya Kikwete. |
Na Dustan Ndunguru,
Songea.
CHAMA cha akiba na mikopo cha Ukombozi Jimbo la Songea (SACCOS)
kilichopo katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, kimekopesha wanachama wake
shilingi bilioni 2.2 katika kipindi cha miaka saba tangu kuanzishwa kwake.
Meneja wa SACCOS hiyo Rainer Ngatunga alisema kuwa fedha hizo
zilizokopeshwa ni kutokana na akiba za wanachama, na sasa chama kina wanachama
1104.
Ngatunga alisema kuwa kati ya fedha hizo shilingi bilioni 1.6
zimekwisha rejeshwa huku akiwataka wanachama wake, watumie fedha wanazokopeshwa
kwa malengo yaliyokusudiwa sambamba na kujenga tabia ya kurejesha mikopo
wanayokopa kwa wakati.
“Kipindi hiki ambacho
msimu wa kilimo unatarajia kuanza wanachama wanapaswa kupeleka maombi ya mkopo
wa kilimo na ada kabla ya Novemba mosi mwaka huu, lakini pia kila mwanachama
ahakikishe anaanzisha miradi ya kiuchumi ili fedha anazokopeshwa aweze
kuelekeza katika eneo husika na kuweza kukuza mtaji wake”, alisema.
Alisema lengo la chama ni kuona kila mwanachama ananufaika na
mikopo inayotolewa ambapo mpaka sasa wengi wao wanaendelea vizuri na shughuli
mbalimbali.
Ngatunga alisema wanajivunia kitendo chao cha kutotegemea kukopa
katika taasisi zingine za kifedha hususani benki, kwani kutokana na hali hiyo
wamekuwa wakiepuka riba kubwa inayotozwa na benki baada ya kukopa hivyo katika kuepukana
na hilo wanachama wahakikishe wanaendelea kuweka akiba zao katika SACCOS yao.
Aliishukuru serikali kwa kuendelea kuhamasisha wananchi wake
kuanzisha vyama vya akiba na mikopo na vikundi vya ujasiriamali, jambo ambalo ni
msaada mkubwa kwa wananchi ambao kimsingi walikuwa wakiogopa kukopa benki
kutokana na riba kuwa kubwa.
No comments:
Post a Comment