Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma, Deusdedith Nsimeki. |
Na Muhidin Amri,
Songea.
JESHI la polisi mkoani Ruvuma, limeagizwa kuwachukulia hatua
madereva wazembe wanaosababisha vifo vya watu wasiokuwa na hatia kunakotokana
na matumizi mabaya ya barabara, kwa kuendesha vyombo vya moto huku wakiwa
wanaongea na simu au kusikiliza muziki wawapo barabarani.
Hatua hiyo ya serikali inatokana na ongezeko kubwa la ajali za
barabarani mara kwa mara, kunakosababishwa na madereva wazembe wasiozingatia
sheria kwa kuongea na simu au kwa kusikiliza muziki kwa kuweka vifaa masikioni,
hali inayomfanya dereva kukosa umakini katika matumizi ya barabara na chombo
anachokiendesha.
Agizo hilo limetolewa juzi mjini Songea na Mkuu wa mkoa huo Said
Mwambungu alipokuwa akifunga kozi fupi za udereva, ufugaji bora wa kuku
na urembo katika chuo cha VETA Songea, ambapo kozi hizo ni mara ya kwanza
kutolewa katika vyuo vinavyomilikiwa na mamlaka stadi ya elimu na
ufundi stadi(VETA) nyanda za juu inayojumuisha mikoa ya Iringa, Njombe na
Ruvuma.
“Polisi kuweni wakali kwa madereva wazembe, nataka kuona mkoa wa
Ruvuma tunapunguza ajali kwa kiasi kikubwa hawa madereva wanaoendesha na
kusikiliza simu siwahitaji katika mkoa wangu, kwani wanasababisha kupungua
kwa nguvu kazi ya taifa hili”, alisema Mwambungu.
Kadhalika amewataka madereva kuwa makini na matumizi ya barabara
na kuomba kuwajali na kuwathamini wenzao wanaotumia barabara hizo hususani
waenda kwa miguu.
Aidha amewahakikishia kwamba wafugaji wa kuku mkoani Ruvuma kwamba
kuna soko kubwa la kitoweo hicho, lakini tatizo kubwa ni kwa wafugaji wenyewe
ambao hawako makini na wanashindwa kuzingatia kanuni za ufugaji bora ili
waweze kuzalisha kuku hao kwa wingi.
Pamoja na mambo mengine akizungumzia kozi ya urembo Mwambungu
aliipongeza VETA kwa ubunifu wa kuibua kozi hiyo, ambayo itasaidia kuongeza ajira kwa wasichana na wavulana wa
mkoa wa Ruvuma.
No comments:
Post a Comment