Monday, October 14, 2013

MJUMBE WA MKUTANO MKUU TAIFA CCM WILAYANI TUNDURU, AKAMATWA NA KIKOSI CHA OPARESHENI OKOA MALIASILI NA KUHOJIWA KWA MASAA NANE


















Na Steven Augustino,
Tunduru.

OPARESHENI Okoa Maliasili inayoendelea kufukuta na kupamba moto katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, imemkumba Mjumbe wa mkutano mkuu wa Chama cha Mapinduzi(CCM) Taifa, Sultani Ajili Kalolo na kuhojiwa kwa zaidi ya masaa nane akiwa anatuhumiwa kushiriki katika vitendo vya ujangili wa kuua Tembo.

Tukio la kukamatwa kwa Mneki huyo lilitokea Oktoba 13 mwaka huu huku wilaya hiyo, ikiwa na kumbukumbu ya kukamatwa kwa bunduki zaidi ya 300 na risasi 667 katika oparesheni zuia ujangili  iliyobatizwa jina la “Wazee wa tintedi”.

Katika tukio hilo Mjumbe huyo wa mkutano mkuu wa CCM taifa (Mneki) Ajili Kalolo alikamatwa akiwa nyumbani kwake eneo la shule  ya msingi Muungano wilayani Tunduru, na kuondoka naye huku.

Baadaye dhamana ilitolewa kwa masharti maalum ambapo hadi kufikia majira ya saa 12 jioni kikosi hicho maalumu kilichokmtia mbaroni, kiliweza kuruhusu ndugu zake wamdhamini kwa masharti ya kwenda kuripoti kituo cha Polisi wilayani humo, Jumatano ya wiki hii.

Akizungumzia tukio hilo kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Deusdedith Nsimeki pamoja na kudai kuwa yeye siyo msemaji wa Oparesheni hiyo Iakini alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kuongeza kuwa watu wanaokamatwa ni wale waliohusika katika matukio hayo pamoja na madalali wa biashara ya meno ya Tembo.

“Unajua mimi siyo msemaji wa Oparesheni hiyo, lakini ninazotaarifa za
Kushikiliwa kwa muda kwa kiongozi huyo wa ngazi ya juu katika Chama
Cha Mapinduzi”, alisema Kamanda Nsimeki na Kuongeza kuwa hali hiyo imetokana na kiongozi huyo kutajwa kuwa ni miongoni mwa Majangili wa Tembo.

Alisema Opareshini hii inatekelezwa kisheria, hivyo haiwezi kumuonea aibu kiongozi ama mtu maarufu hivyo wote wanaokamatwa wamekuwa wakitajwa kuwa miongoni  mwa wahusika kwa namna moja na matukio ya vitendo vya kijangili hivyo oparesheni hiyo haitawaonea watu wasio husika.

Kamanda Nsimeki aliendelea kueleza kuwa Oparesheni hiyo iliyopewa jina la Okoa maliasili inayoendelea wilayani Tunduru, pamoja na kuenea karibu nchi nzima, kwa kujumuisha mikoa husika pia inaendelea katika wilaya ya Namtumbo katika Kijiji cha Likusenkuse na Liparamba wilayani Mbinga lengo ikiwa ni kukomesha vitendo vya ujangili wa mauaji ya Tembo na maliasili nyingine za Tanzania.

Alisema Oparesheni hiyo inahusisha vyombo mbalimbali vya majeshi ya ya ulinzi katika nchi yetu, wamo pia askari wa jeshi la wananchi wa Tanzania, usalama wa taifa, uhamiaji na Polisi ambao kwa pamoja wanapitia taarifa mbalimbali na kuwakamata watu wote ambao wanakuwa wakitajwa kujihushisha na matukio ya ujangili.

Kwa mujibu wa taarifa za oparesheni iliyofanyika Agosti mwaka 2012
iliyoendeshwa chini ya usimamizi wa serikali, kwa ajili ya kuzuia vitendo vya uhalifu na ujangili  iliyofanyika wilayani Tunduru mkoani Ruvuma jumla mali zenye thamani ya milioni 618.408, bunduki zaidi ya 300 na risasi  667 na maganda ya risasi 150 zilikamatwa baada ya kubainika kuwa zinamilikiwa kinyume cha sheria.   

No comments: