Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga, naye alisisitiza kwa kuwataka Polisi kuacha kupiga raia na endapo watafanya hivyo, wataonekana kama ni watu ambao wanajitawala wao wenyewe. |
Baadhi ya wananchi nao walihudhuria siku hiyo ya uzinduzi. |
Vikundi vya ngoma navyo havikuwa mbali katika kutumbuiza. (Picha zote na Gwiji la matukio mkoani Ruvuma) |
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
WITO umetolewa kwa Askari Polisi wilayani Mbinga mkoa wa
Ruvuma, kuacha kupiga raia na endapo watafanya hivyo, wataonekana kama ni watu
ambao wanajitawala wao wenyewe.
Sambamba na hilo wametakiwa kujenga ushirikiano na wananchi
ili kuweza kuleta ufanisi katika utendaji wa kazi zao kila siku, kwa lengo la
kuimarisha usalama kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga, alisema hayo alipokuwa
mgeni rasmi akizungumza kwenye uzinduzi wa mradi wa kikosi kazi (task force)
tarafa ya Mbinga mjini.
Ngaga alisema mradi huo wa kikosi kazi ndani ya tarafa hiyo ambao
umeanzishwa hapa wilayani, hauna budi uwe endelevu kwa lengo la kuimarisha kazi
zinazofanywa na askari kata, mkuu wa tarafa na vikundi vingine vinavyofanya
kazi za kila siku katika kushughulikia miradi mingine ya polisi jamii, ndani ya
tarafa nyingine zilizopo mkoani humo.
“Polisi wakirahisishiwa kazi katika ngazi ya tarafa, ulinzi
utakuwa ukiimarika kwa kiasi kikubwa, ikiwemo suala hili la utii bila shuruti nalo
nina imani kubwa wananchi nao watakuwa na uelewa mkubwa zaidi”, alisema Ngaga.
Aidha alisisitiza Viongozi na wananchi kwa ujumla kuendeleza
ushirikiano na hawatakiwi kurudi nyuma kwenye jambo hili, kwa kile alichoeleza
kuwa kuanza kwa uzinduzi huo, ni mwanzo mzuri ambao unahitaji uwe endelevu na
sio vinginevyo.
Naye Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Deusdedit Nsimeki
kabla ya kufanya uzinduzi huo alisema, Serikali itaendelea kuboresha mazingira
ya utendaji kazi kwa Jeshi la polisi, lakini mpango wa kuendelea
kuwashughulikia wahalifu hususani pembezoni(mipakani) na maeneo mengine ndani
ya nchi, utabaki palepale.
“Ndugu zangu sisi kwa upande wa jeshi la polisi tumejipanga
katika hili, wahalifu wengi ni vijana wetu huko katika kata zetu, kinachotakiwa
hapa tuwaelimishe hawa vijana waachane na mambo haya”, alisisitiza Nsimeki.
Awali akisoma taarifa kwa niaba ya Mkuu wa polisi wa wilaya
ya Mbinga, Mkaguzi mkuu wa tarafa hiyo Inspekta Nassibu Kassim Sued alisema
kuwa mradi huo wa kikosi kazi unajumuisha maafisa na askari husika ambao
watakuwa na majukumu ya kiutendaji wa kipolisi katika tarafa, kiungo kati ya
polisi na wananchi.
Kadhalika alieleza kuwa kuweka kumbukumbu za wahalifu sugu na
wazoefu wa ndani ya tarafa, kukusanya taarifa za kiintelijensia kutoka kwa
watoto na walimu mshuleni na hata, kutafuta mbinu za kuwashirikisha vijana
katika miradi ya polisi jamii.
Nassibu alisema, ni ukweli usiopingika kwamba Polisi hawawezi
kufikia malengo husika ya ulinzi shirikishi katika jamii, endapo hawatatimiza
dhana ya kushirikisha wananchi hasa tukiamini kwamba jukumu la ulinzi katika
nchi hii, ni la kila mwananchi kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 28 (1) ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Hata hivyo Mkuu huyo
wa tarafa alieleza changamoto wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa mradi
huu, ni pamoja na kukosa miundombinu kwa maana ya usafiri na vifaa vingine
husika, ambavyo vingeweza kuwarahisishia polisi katika utendaji wao wa kazi za
kila siku.
No comments:
Post a Comment