Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
VURUGU zilizodumu kwa masaa matano zimejitokeza katika kijiji
cha Lipilipili kata ya Mpepai wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, na askari wa nne
wa Jeshi la mgambo wilayani humo akiwemo ofisa mtendaji wa kijiji hicho, wamenusurika
kuuawa kufuatia wananchi wenye hasira kali, kuwashambulia wakiwa kwenye
majukumu yao ya kazi.
Hali hiyo imejitokeza majira ya saa 1:30 asubuhi, Oktoba 7
mwaka huu ambapo mgambo na mtendaji huyo walikwenda
kijijini hapo kutekeleza azimio la kikao cha kamati ya maendeleo ya kata hiyo,
ambacho kilifikia uamuzi wa waliokataa katani humo kuchangia shughuli za ujenzi
wa maabara na bweni la kulala wanafunzi katika shule ya sekondari Dokta Shein,
wakamatwe na kuchangia kila mmoja shilingi 25,000 ya mchango husika.
Akizungumza na waandishi wa habari, ofisa mtendaji wa kata ya
Mpepai Anssila Kumburu alisema, katika kikao cha kamati hiyo kilichoketi kijiji
cha Luhangai Septemba 27 mwaka huu, Mwenyekiti wa kamati ambaye ni Diwani wa
kata hiyo Francis Nchimbi ndiyo yeye aliyetangaza uamuzi huo wa kuleta mgambo,
kwa ajili ya kusaidia kuwasaka wale wote waliokataa kuchangia miradi hiyo ya maendeleo.
Kumburu alisema Septemba 30 mwaka huu ndipo mgambo hao
walianza kutekeleza jukumu hiyo kwa kushirikikiana na maofisa watendaji wa
vijiji vya kata ya Mpepai, kupita kwa kila kaya kukusanya michango husika
ambapo kati ya vijiji vitano vya kata hiyo, vijiji vinne walivyopita hapakuwa
na tatizo lolote lile wananchi wake waliitikia wito huo kwa kutoa michango
waliyoelekezwa.
Kufikia Oktoba 7 mwaka huu wakiwa kitongoji cha Mtukula
kijiji cha Lipilipili katani humo, Mgambo tisa wakiwa na ofisa mtendaji wa
kijiji hicho Petro Mayowa walishambuliwa na wananchi kwa kupigwa seheme mbalimbali
za mwili kwa kutumia silaha za jadi.
Alifafanua kuwa baada ya tukio hilo wananchi hao walimchukua
Ofisa mtendaji wa kijiji hicho na kumpeleka ofisini kwake, ambako walimwingiza
ndani na kumfungia huku wakiwa tayari wamemjeruhi vibaya maeneo ya kichwani
huku akivuja damu kwa wingi.
“Kutokana na tukio hili la kufungiwa ndani, wasamaria wema
walijitokeza baada ya masaa mawili na kuvunja mlango wa ofisi hiyo wakati
majeruhi alipokuwa akipaza sauti za kuomba msaada”, alisema Kumburu.
Kufuatia tukio hilo ambalo ofisa mtendaji huyo aliripoti
polisi akiwa na majeruhi ambao ni mgambo, Loy Mbunda, Joseph Alli, Kanisius
Ngonyani, Agness Mwilafi na mtendaji huyo wa kijiji ambapo baadaye walifikishwa
katika hospitali ya wilaya ya Mbinga kwa ajili ya matibabu.
Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Robert
Elisha, pamoja na kukiri kupokea majeruhi hao alisema walipatiwa matibabu
ambapo mtendaji wa kijiji cha Lipilipili Petro Mayowa, ambaye aliumizwa vibaya alishonwa kichwani na hao wenzake ambao
waliumizwa sehemu mbalimbali za miili yao walipatiwa matibabu na kuruhusiwa.
Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma, limethibitisha kutokea kwa
tukio hilo ambapo Kamanda wa polisi wa mkoa huo Deusdedit Nsimeki alisema baada
ya polisi kupata taarifa ya tukio hilo walikwenda huko na kufanikiwa kuwakamata
wanakijiji wa nane ambao wanadaiwa kuhusika na vurugu hizo.
Nsimeki aliwataja watuhumiwa kuwa ni Bonventure Kapinga, John
Nchimbi, Kondrad Haulle, Willson Kapinga, Thomas Kapinga, Maiko Kapinga,
Zackaria Ndunguru na Amos Ndunguru.
Alieleza kuwa wanakijiji hao walitumia silaha aina ya Panga,
magongo na fimbo za mianzi kuwapiga mgambo hao na kwamba polisi wanaendelea
kuwahoji na upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma
zitakazowakabili.
No comments:
Post a Comment