Na Muhidin Amri,
Songea.
WAHITIMU kidato cha nne, shule ya sekondari Beroya iliyopo Manispaa
ya Songea mkoani Ruvuma ambao wanatarajia kufanya mitihani yao ya mwisho, Novemba
mwaka huu wametakiwa kujiepusha na udanganyifu wa kutafuta majibu ya mitihani
hiyo, badala yake watumie muda uliobaki kujisomea ili waweze kufanya vizuri na
kufaulu kwa kupata alama za juu.
Aidha wameelezwa kuwa, serikali tayari imejipanga kudhibiti
vitendo hivyo ili kuwadhibiti wanafunzi wenye tabia hiyo na kwamba wameshauriwa
kutumia muda huu mfupi uliobakia, kujikumbusha yale waliyosoma na kufundishwa
na walimu wao ili siku ya mwisho ya mitihani yao waweze kufuzu vigezo husika.
Ofisa elimu sekondari katika Manispaa hiyo, Leo Mapunda
alisema hayo alipokuwa akizungumza na wanafunzi, walimu na wazazi katika
mahafali ya saba kidato cha nne, shule ya sekondari Beroya yaliyofanyika juzi
mjini hapa.