Madiwani wa Halmashauri ya mji wa Mbinga na baadhi ya waalikwa wakitoka nje ya ukumbi baada ya kikao cha baraza la Madiwani hao kuvunjika. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, kikao cha baraza la
Madiwani wa Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, kimeshindwa kufanyika
na badala yake kimevunjika kufuatia Madiwani hao kumkataa Mkurugenzi mtendaji
wa halmashauri hiyo, Robert Kadaso Mageni wakidai kuwa hawataki kufanya naye
kazi tena kutokana na Mkurugenzi huyo kushindwa kusimamia kikamilifu miradi ya
maendeleo ya wananchi wa halmashauri hiyo.
Madiwani hao walichukua maamuzi hayo magumu leo katika kikao hicho
ambacho walitakiwa kupokea taarifa za maendeleo ya wananchi, robo ya kwanza ya
mwaka kilichoketi kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa.
Aidha maamuzi hayo yalifikiwa baada ya Mwenyekiti wa Madiwani
hao, Kipwele Ndunguru kufungua kikao cha baraza hilo na kuwataka Madiwake wake
wapokee agenda za kikao, ambapo kwa pamoja walimkatalia kupokea agenda hizo
huku wakieleza kuwa wapo tayari kuzipokea endapo Mkurugenzi huyo hatakuwepo
katika baraza hilo.
“Sisi tupo tayari kuendelea na baraza hili endapo Mkurugenzi
huyu atupishe humu ndani akaendelee na kazi zake, mangapi tumezungumza kwa
ajili ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya wananchi utekelezaji wake umekuwa
ni tatizo tunataka ndani ya baraza hili atupishe aondoke”, alisema Benedict
Ngwenya Diwani wa kata ya Mpepai.
Akichangia hoja katika baraza hilo naye Tasilo Ndunguru
ambaye ni Diwani wa kata ya Kikolo alisema kuwa hawataki kuiona sura ya
Mkurugenzi huyo katika baraza la Madiwani wa mji wa Mbinga, huku akieleza kuwa
ameshindwa hata kusimamia mradi wa uvunaji msitu wa Mbambi na kusababisha
hasara ya mamilioni ya fedha hivyo hawaoni sababu ya kuendelea kuwa naye katika
halmashauri ya mji huo.
Mkurugenzi huyo pamoja na kujikuta akiwa katika wakati mgumu
kwa upande wake alipopewa nafasi ya kujieleza alisema kuwa yeye akiwa Katibu wa
kikao hicho, anachotambua ni kwamba kilichopo mbele ya baraza ni kupokea agenda
na kwamba kama wajumbe hao wamekataa kuzipokea maana yake hakuna kikao.
“Tukiendelea kujadili yaliyopo hapa sura yangu hayatasaidia
kwamba sisi ni binadamu ni kweli tumeumbwa na chuki lakini vilevile na kusamehe,
mimi katika nafasi yangu ni Katibu wa kikao hiki nina hiari ya kumkaimisha mtu
au kutokaimisha”, alisema Mageni.
Hata hivyo katika kikao hicho ambacho kilihudhuriwa na Mkuu
wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye pamoja na kuwasihi Madiwani hao wasifanye
hivyo, lakini hawakuweza kukubaliana naye badala yake waliendelea kujenga msimamo
wao wa kukataa kufanya kikao hicho na hatimaye Mwenyekiti wa baraza hilo, Ndunguru
alilazimika kuvunja baraza na Madiwani walitoka nje ya ukumbi na kurudi makwao.
No comments:
Post a Comment