Na Albano Midelo,
Songea.
MTAA wa Mitendewawa na Chandarua iliyopo katika Manispaa ya
Songea mkoani Ruvuma, wananchi wake wanatarajia kunufaika na kuondokana na adha ya upatikanaji wa maji safi na salama, baada ya serikali
kuanza kujenga mradi wa maji wenye thamani ya shilingi milioni 517.
Samwel Sanya ambaye ni Mhandisi wa Maji katika Manispaa hiyo alisema
hayo mbele ya Mkuu wa wilaya ya Songea, Palolet Mgema wakati Mkuu huyo wa
wilaya alipofanya ziara yake ya ukaguzi wa mradi huo.
Alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo ulitakiwa kuanza mwaka
wa fedha wa 2014/2015 lakini utekelezaji wake haukufanikiwa kutokana na fedha
hizo kuchelewa kuwafikia kutoka Serikali kuu.
Mhandisi Sanya alisema utekelezaji wa mradi huo ambao una
urefu wa kilometa 13.4 ukiwa na vituo 13 vya maji, umeanza katika mwaka wa
fedha wa 2016/2017 ambapo Mkandarasi husika amefikia zaidi ya asilimia 60 ya utekelezaji
huo.
Alifafanua kuwa kisima cha mradi huo kina urefu meta 68 na
kwamba uwezo wake ni kuzalisha maji lita 7,000 kwa saa moja ambapo wanufaika wa
mradi watakuwa wakazi zaidi ya 840 katika mitaa hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Songea mara baada ya kuukagua
alimtaka Mhandisi huyo kuhakikisha kwamba mradi unajengwa kwa ubora unaotakiwa
na kumaliza ujenzi kwa wakati uliopangwa.
Mkoa wa Ruvuma unakadiriwa kuwa na wakazi 1,497,853 kati ya
hao ni wakazi 851,034 sawa na asilimia 57 tu ndiyo wanaopata maji safi na
salama, kwa mujibu wa takwimu za hadi kufikia Oktoba mwaka jana.
No comments:
Post a Comment