Na Yeremias Ngerangera,
Namtumbo.
WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Namtumbo mkoa
wa Ruvuma wamemchagua, Aggrey Mwansasu kuwa Mwenyekiti mpya wa CCM wilayani
humo baada ya kumbwaga chini aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Benjamini
Nindi.
Uchaguzi wa kumpata Mwenyekiti huyo ulifanyika juzi kwenye
ukumbi wa shule ya Sekondari Namtumbo, ambayo inamilikiwa na Jumuiya ya wazazi ya
Chama Cha Mapinduzi iliyopo mjini hapa.
Katika uchaguzi huo awali uliingia dosari baada ya msimamizi
wa uchaguzi huo, Zena Mijinga kujisahau kwa kutosoma kanuni ya ushindi wa uchaguzi
huo ambapo mgombea ni sharti apate kura zaidi ya nusu ya wapiga kura waliopo
kwenye uchaguzi huo.
Kutosomwa kwa kanuni hiyo na wagombea hao wa nafasi hiyo
kutofikia nusu ya kura zilizopigwa iliwataka wajumbe wa mkutano huo kurudia
kupiga kura kwa nafasi hiyo ya Mwenyekiti, jambo ambalo liliibua hasira kutoka
kwa wajumbe wakidai kwamba hali hiyo inaonesha kutaka kumbeba mgombea mmojawapo
katika uchaguzi huo huku wakiongeza kuwa kanuni hiyo kwa nini haikusomwa kabla
ya uchaguzi.
Mwenyekiti wa muda wa mkutano huo, Fadhil Kitete alionekana
kuokoa jahazi kutoka kwa baadhi ya wajumbe waliotaka kukataa kurudia kwa uchaguzi
huo huku akiwaomba wajumbe hao radhi kwa kutosoma kanuni hiyo kabla ya uchaguzi
na kusema kuwa ni kosa la kibinadamu limefanyika na kwamba aliwataka wajumbe
waridhie kurudia kupiga kura kwa nafasi hiyo ya Mwenyekiti kwa kuzingatia
kanuni hiyo.
Kitete aliongeza kuwa kanuni ndiyo siku zote inayoongoza
uchaguzi na kurudia uchaguzi ambapo haitazuia wajumbe kumchagua mgombea wanayemtaka.
Baadaye wajumbe kwa pamoja walikubaliana na hoja hiyo na
hatimaye kuweza kupiga kura na kumchagua Mwenyekiti wa CCM wilayani humo ambaye
walimtaka.
Waliogombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Cha
Mapinduzi wilayani Namtumbo walikuwa wanne ambao ni Legani Luambano, Yordani
Fusi, Benjamini Nindi na Aggrey Mwansasu ambapo katika uchaguzi
wa awali Legani Luambano alipata kura 20, Yordani Fusi alipata kura 25,
Benjamini Nindi aliyekuwa akitetea kiti hicho alipata kura 290 na
Aggrey Mwansasu alipata kura 304 kati ya kura 645 zilizopigwa.
Uchaguzi wa marudio uliwashindanisha wagombea
wawili Benjamini Nindi na Aggrey Mwansasu ambao walionesha kuwa na
ushindani mkubwa kwa wajumbe, lakini mpaka mwisho wa uchaguzi huo
msimamizi wa uchaguzi huo Zena Mijinga alimtangaza Aggrey Mwansasu
kuwa mshindi kwa nafasi ya Mwenyekiti kwa kumbwaga
mpinzani wake Benjamini Nindi aliyekuwa anatetea nafasi
hiyo.
Mijinga alimtangaza Aggrey Mwansau kuwa
ameshinda nafasi hiyo kwa kupata kura 369 dhidi ya kura 228 alizopata mpinzani
wake kati ya kura 610 zilizopigwa ambapo kura 13
ziliharibika katika uchaguzi huo.
Hata hivyo katika mkutano huo pia walichaguliwa wajumbe wawakilishi
wa mkutano mkuu wa Taifa, mkutano mkuu wa mkoa na viongozi
wa nafasi ya katibu wa siasa itikadi na uenezi, jumuiya ya wanawake,
vijana na wazazi.
No comments:
Post a Comment