Na Mwandishi maalum,
Mbinga.
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM)
wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, Sostenes Nchimbi amewaomba Wadau mbalimbali
waliopo wilayani humo kujitokeza kwa wingi na kuchangia maendeleo ya shule ya sekondari
ya wazazi Mkinga iliyopo katika wilaya hiyo.
Ombi hilo lilitolewa juzi na Mwenyekiti huyo wakati alipokuwa
ametembelea shule hiyo huku akiwa ameambatana na viongozi wengine wa jumuiya
hiyo kwa lengo la kujionea maendeleo yake na changamoto mbalimbali.
“Tumeingia madarakani kwa lengo la kuweza kuisaidia jamii
iweze kusonga mbele kimaendeleo siku zote umoja ni nguvu utengano ni udhaifu,
napenda kueleza kwamba nipo tayari kuunga mkono katika maendeleo ya shule hii”,
alisema Nchimbi.
Awali akizungumzia juu ya changamoto zinazoikabili shule ya sekondari
ya wazazi Mkinga, Mkuu wa shule hiyo Francis Hyera alisema kuwa shule hiyo
inakabiliwa na tatizo la uchakavu wa miundombinu ya majengo ambapo yanapaswa
kufanyiwa ukarabati ili yaweze kuwa katika hali nzuri.
Pia Hyera aliongeza kuwa katika shule hiyo vyoo vya wanafunzi
vimejaa hivyo watoto wanaosoma hapo wanapata shida wakati wa kwenda kujisaidia
haja kubwa na ndogo.
“Shule hii ina uhai mzuri kitaaluma, maendeleo yake ni mazuri
kwa mwaka jana ufaulu wa mtihani wa mwisho kidato cha nne hatukuwa na daraja
sifuri na mtihani wa mwaka huu, tunatarajia tuwe pia na matokeo mazuri”,
alisema Hyera.
Kwa ujumla shule hiyo ilianzishwa mwaka 1979 na kwamba mpaka
sasa ina jumla ya wanafunzi 200 kutoka kidato cha kwanza hadi cha nne ambapo inamilikiwa
na Jumuiya ya Wazazi ya CCM wilaya ya Mbinga, lakini inahitaji ukarabati mkubwa
wa miundombinu yake ili iweze kuwa endelevu.
No comments:
Post a Comment