Imeelezwa kuwa kati ya wagonjwa 104 walioripotiwa, 20
wamefariki dunia, ambapo taarifa iliyotolewa jana Jumanne na Ofisa Habari wa Wizara
hiyo, Catherine Sungura imesema kuwa Shirika la Afya Duniani (WHO) limeeleza
nchini Madagascar mikoa minane imeripotiwa kuwepo wagonjwa ukiwemo mji
mkuu wa nchi hiyo, Antananarivo.
Ugonjwa huo ulianza kuripotiwa Agosti 23 hadi Septemba 28
mwaka huu.
“Wengi walioripotiwa wameonyesha kuwa na uhusiano kwa njia
moja au nyingine na mgonjwa wa kwanza jambo linalothibitisha yapo maambukizi ya
ugonjwa wa tauni kati ya binadamu na binadamu.
Hivyo kwa mujibu wa WHO, ipo hatari ya wastani (Moderate
risk) ya ugonjwa huo kusambaa katika nchi jirani na Madagascar,” imesema
taarifa hiyo.
Wizara imesema tahadhari hiyo inatolewa kwa kuzingatia
kwamba, Madagascar haiko mbali sana na Tanzania na inawezekana kukawa na
mwingiliano kati ya wananchi wa nchi hizi mbili.
“Serikali inasisitiza kuwa mpaka sasa ugonjwa wa tauni
haujaingia nchini. Kwa kuwa magonjwa hayaangalii mipaka, tunahitaji kuchukua
tahadhari madhubuti ili kuzuia ugonjwa huu usiingie nchini.
Hivyo wananchi wanahimizwa kuzingatia kanuni za afya za
kuzuia ugonjwa huu, pia wanatakiwa kuripoti haraka kwenye vituo vya huduma za
afya waonapo dalili zozote za ugonjwa huu,” imesema wizara.
Sungura amesema hatua zilizochukuliwa baada ya kupata taarifa
ya tahadhari ya Shirika la Afya Duniani, Septemba 29 mwaka huu wamesambaza
barua za tahadhari ya ugonjwa huo kwa Makatibu tawala wa mikoa yote ya Tanzania
Bara.
Makatibu tawala katika barua hizo wametakiwa kuchukua
tahadhari ikiwa ni pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa katika viwanja
vya ndege, mipakani na bandari ili kubaini wagonjwa waingiao nchini wakiwa na
dalili za ugonjwa huo.
“Kupitia kwa waganga wakuu wa mikoa na wilaya, Wizara inatoa
maelekezo ya kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na utambuzi wa magonjwa katika
vituo vya kutolea huduma,” amesema.
Pia, Wizara itatoa elimu kwa jamii kuhusu ugonjwa huo.
Kuhusu tauni;
Ugonjwa huu husababishwa na bakteria anayejulikana kitaalamu,
“Yersinia pestis” ambaye hupatikana katika baadhi ya wanyama wadogo kama vile
panya, paka, mbwa na viroboto.
Taarifa hiyo imezitaja njia kuu tatu ambazo mtu anaweza
kupata maambukizi kuwa ni kung’atwa na viroboto vyenye maambukizi ya bakteria
hao kutoka kwa wanyama kama vile mbwa na paka ambao huweza kubeba viroboto.
“Kugusana bila kuwa na kinga mwili na majimaji yenye vimelea
vya bakteria kutoka kwa mtu au mnyama aliyeathirika kwa njia ya kugusa sehemu
zenye vimelea zilizochafuliwa na mgonjwa au mnyama na kisha mtu huyo kujigusa
mdomoni au puani”, imesema taarifa hiyo.
Njia nyingine ni kugusana na majimaji yanayotoka kwa mgonjwa
kwa njia ya kukohoa au kupiga chafya bila ya mgonjwa kufunika pua au mdomo. (Muungwana Blog)
No comments:
Post a Comment