Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Pombe Magufuli. |
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
SAKATA la tuhuma wizi wa mamilioni ya fedha za mradi wa uvunaji wa
msitu wa Mbambi katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, limeibua sura
mpya baada ya wananchi wa kata ya Matarawe mjini hapa kuitaka halmashauri hiyo
iwalipe asilimia 10 ya fedha za mapato yaliyotokana na msitu huo.
Asilimia hiyo ya mapato wanayodai wananchi hao imeelezwa kuwa
ni makubaliano yaliyofanywa katika vikao halali vilivyopita na kupitishwa na baraza
la Madiwani wa halmashauri ya mji huo.
Walisema wanamshangaa Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya
mji wa Mbinga, Robert Kadaso Mageni kwa kutosimamia kikamilifu fedha za msitu
huo na kusababisha wizi huo ufanyike na wao kukosa sehemu ya mapato yao.
Hayo yalisemwa juzi na wananchi hao katika kikao cha kujadili
maendeleo yao ya kata hiyo kilichofanyika katani humo ambacho kilikuwa na
majadiliano pia ya ujenzi wa vibanda vya soko la kata ya Matarawe.
Mwenyekiti wa kata hiyo, Philibert Hyera alisema kuwa msimamo
waliokuwa nao wanataka walipwe sehemu ya asilimia 10 iliyotokana na mapato ya fedha za uvunaji wa msitu wa Mbambi kwani wao ndio walioshiriki kwa miaka mingi kuutunza
msitu huo.
“Sisi tunataka pia hata magogo ya miti na mbao zilizobakia
kule msituni, halmashauri itupatie ili ziweze kutusaidia katika shughuli zetu
za maendeleo ya kata”, alisisitiza Hyera.
Naye Diwani wa kata hiyo, Leonard Mshunju aliongeza kuwa
maadhimio na michango yote iliyotolewa na wananchi wa kata yake atayafikisha
kwenye kikao cha baraza la Madiwani kitakachoketi Novemba 27 mwaka huu ili
kuweza kufikia muafaka na kufanyiwa utekelezaji.
Awali hivi karibuni kufuatia sakata hilo la uvunaji wa msitu
huo, baraza la Madiwani la halmashauri hiyo lilitoa pendekezo lake la kumkataa
Mkurugenzi huyo wa halmashauri hiyo, Mageni kwamba hawataki kufanya naye kazi tena
wakimtuhumu ametafuna fedha za mauzo ya mbao zilizopasuliwa katika msitu huo na
kulipotosha baraza kwa kutoa taarifa za uongo juu ya mapato yaliyotokana na
uvunaji uliofanyika huko msituni.
Kufuatia upotoshaji huo anaotuhumiwa kulidanganya baraza hilo,
anadaiwa kusababisha halmashauri iweze kupata hasara ya shilingi milioni
888,000,000 na kumuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe
Magufuli amchukulie hatua za kinidhamu ikiwemo ahamishwe haraka hawataki
kufanya naye kazi.
Maamuzi hayo ya baraza hilo yalifikiwa baada ya Kamati maalum iliyoundwa na Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye kutoa taarifa yake ya uchunguzi katika baraza la dharula lililoketi Novemba 20 mwaka huu, kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa, ambapo baada ya kufanya uchunguzi wake waliweza kubaini mapungufu yaliyojitokeza katika shughuli hiyo ya uvunaji wa msitu wa Mbambi.
Maamuzi hayo ya baraza hilo yalifikiwa baada ya Kamati maalum iliyoundwa na Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye kutoa taarifa yake ya uchunguzi katika baraza la dharula lililoketi Novemba 20 mwaka huu, kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa, ambapo baada ya kufanya uchunguzi wake waliweza kubaini mapungufu yaliyojitokeza katika shughuli hiyo ya uvunaji wa msitu wa Mbambi.
No comments:
Post a Comment