Mratibu wa Udhibiti wa Chakula na Dawa (TFDA) katika Manispaa ya Songea, Vitalis Mkomela akionesha dawa za aina mbalimbali kwa waandishi wa habari ambazo zimepita muda wake wa matumizi. |
Na Albano
Midelo,
Songea.
MAMLAKA ya Udhibiti wa Chakula na Dawa (TFDA) katika Manispaa
ya Songea Mkoa wa Ruvuma, imekamata dawa za binadamu ambazo zilikuwa
zinaendelea kuuzwa zikiwa zimepita muda wake katika baadhi ya maduka ya dawa
muhimu yaliyopo mjini hapa.
Mratibu wa TFDA katika Manispaa hiyo, Vitalis Mkomela alisema
kuwa dawa za aina mbalimbali zenye thamani ya shilingi 244,000 zilikamatwa
katika operesheni maalum ambayo ilifanywa na watalaamu wa idara ya afya.
Mmiliki wa duka moja ambalo lilikutwa na dawa hizo amekiri
kuuza dawa hizo zilizomalizika muda wake na kwamba tayari amepigwa faini ya
shilingi 600,000.
Mamlaka hiyo inatoa rai kwa wananchi wa Manispaa ya Songea
wanaponunua dawa kusoma kwanza maelekezo, yakiwemo yale ambayo yanaonesha dawa
zilitengenezwa mwaka gani na tarehe ya mwisho wa matumizi.
Mkomela alisema kuwa raia mmoja ambaye alikwenda kununua dawa
na kubaini aliuziwa dawa ambazo muda wake umepita ndipo aliweza kuisaidia TFDA
kufanya ufuatiliaji na kuweza kufanikiwa kukamata dawa hizo ambazo zinaweza
kuleta madhara makubwa kwa binadamu.
Alisisitiza kuwa TFDA itaendelea kufanya operesheni za
kushitukiza na kukagua maduka ya dawa na vipodozi katika Manispaa ya Songea
hiyo.
Katika Manispaa ya Songea pia TFDA imekamata diapers (Nepi)
ambazo muda wake umemalizika tangu Agosti mwaka huu zikiendelea kuuzwa katika baadhi
ya maduka yaliyopo Soko kuu la Songea mjini.
Mratibu huyo wa TFDA katika Manispaa hiyo alisema wamekamata
Nepi aina ya Ponpon 65 zenye thamani ya shilingi 277,500 ambapo mmiliki husika
naye alikiri kuuza bidhaa hizo ambazo muda wake umepita hivyo alipigwa faini ya
shilingi zaidi ya lakini moja ikiwemo na gharama za kuteketeza mzigo huo.
No comments:
Post a Comment