Eliezer Nyoni Mwenyekiti Baraza huru la wazee Manispaa ya Songea. |
Na Albano Midelo,
Songea.
WAZEE katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma
wameiomba Serikali kutatua kero ya kupata matibabu bure, ambayo inaongoza kwa
wazee wa Manispaa hiyo hali ambayo inasababisha wengi wao kukosa matibabu.
Akisoma risala ya maadhimisho ya siku ya wazee duniani Oktoba
Mosi mwaka huu, Makamu Mwenyekiti wa Baraza Huru la Wazee wa Manispaa ya Songea
Sophia Hasara, alisema ni muhimu sasa kwa Serikali kuwapatia wazee hao kadi za
matibabu bure kama ilivyoelekezwa hapo awali ili waweze kuondokana na kero hiyo
pale wanapokwenda kupatiwa matibabu katika vituo vya serikali.
Hasara alisema kuwa kuna umuhimu kwa Manispaa hiyo kuharakisha
mchakato wa upatikanaji wa kadi hizo kwa wazee wote ili kuweza kumaliza kero
hiyo ambayo imedumu kwa muda mrefu na sasa inasababisha baadhi ya wazee
kupoteza maisha kutokana na wakati mwingine wanashindwa kugharamia matibabu.
Wazee hao pia wameipongeza Serikali ya awamu ya tano chini ya
Rais Dokta John Magufuli kwa kuongeza bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 ambapo walisema
bajeti hiyo itawanufaisha kwa kuweza kupata matibabu wazee wa hapa nchini.
Vilevile katika risala yao wazee hao wamelaani matukio ya
mauaji ya wazee, utekaji nyara wa watoto na mashambulio mbalimbali yanayotokea
kwa viongozi na kwamba ili kukabiliana na matukio hayo wameshauri Serikali
kukaa na wazee ili waweze kupata mawazo ya nini cha kufanya katika kuondoa changamoto hizo.
Walisema kuwa Serikali inapaswa kuwashirikisha wazee wa kada
mbalimbali ili waweze kutumia ujuzi, uzoefu na michango ya mawazo yao katika
kufanikisha malengo ya serikali.
Kadhalika walifafanua kuwa ingawa wazee hao hawana nguvu
nyingi, hata hivyo kwa kutumia hekima na busara zao wanaweza kuelekeza, kushauri
na kusimamia kwa ufanisi lengo kuu la awamu ya tano la kuwa na Serikali ya viwanda
ili kuleta maendeleo kwa Watanzania.
Wazee hao wamesisitiza mshikamano, umoja na juhudi ili
kufikia lengo lililowekwa na Serikali la Hapa kazi tu na kusisitiza kwamba itunge
sheria ya wazee ili kuwezesha kunufaika na sheria hiyo kwa kuwa sera ya wazee
pekee yake haina uwezo wa kutatua changamoto zao.
“Sisi wazee wa Manispaa ya Songea hatujanufaika lolote na
sera ya Taifa ya wazee ya mwaka 2003 kwa sababu sera hiyo haina meno kwa kuwa
haijatungiwa sheria yenye nguvu’’, walisema kupitia risala yao.
Pia wamemuomba mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Mbunge wa
Songea mjini, Leonidas Gama kuwafikishia kilio chao Bungeni na kwamba hawaoni
sababu ya msingi ya kucheleweshewa kutungiwa sheria hiyo wakati sera imedumu kwa
muda mrefu.
Kulingana na takwimu za wazee mwaka 2016, Manispaa hiyo ina
zaidi ya wazee 11,000 hivyo katika maadhimisho hayo ya mwaka huu 2017 ni ya 19 ambapo
maadhimisho ya kwanza yalifanyika mwaka 1999 na kauli mbiu ya mwaka huu ni kuelekea
Uchumi wa Viwanda, Tuthamini Mchango, Uzoefu na Ushiriki wa Wazee kwa Maendeleo
ya Taifa.
No comments:
Post a Comment