Washiriki wa mchezo, mpira wa miguu wakiwa katika picha ya pamoja siku ya tukio la tamasha la michezo katika tarafa ya Namswea wilayani Mbinga. |
Na Mwandishi wetu,
Mbinga.
KATIKA kuenzi utamaduni wa
kiafrika, Wananchi wanaoishi katika tarafa ya Namswea wilaya ya Mbinga mkoani
Ruvuma wamefanya tamasha la michezo mchanganyiko ndani ya tarafa hiyo, ikiwa ni
lengo la kuhamasisha shughuli mbalimbali za maendeleo.
Tamasha hilo lilizinduliwa
hivi karibuni katika viwanja vya michezo Namswea likiwa limebeba kauli mbiu “Ujana ni hazina tuutumie vizuri kwa
manufaa ya sasa na baadae” ambapo lilifadhiliwa na Thotnant Ezekiel Kayombo
ambaye alikuwa mgeni rasmi huku michezo iliyokuwa ikichezwa siku hiyo ni
mpira wa miguu na ngoma mbalimbali za asili.
Akizungumza na mwandishi
wetu, Kayombo alifafanua kuwa lengo la tamasha hilo ni kufikisha ujumbe huo kwa
jamii hasa vijana juu ya wajibu wao katika kushiriki kwenye shughuli za
kimaendeleo katika maeneo yao wanayoishi.
Kayombo alisema kuwa
msisitizo umewekwa pia katika shughuli za upandaji miti ya mbao na ile ambayo
inatunza mazingira hasa katika vyanzo vya maji.
“Lengo ni kupanda miti laki
tatu kila mwaka katika tarafa hii kwa miaka sita kuanzia sasa hadi mwaka 2022,
muda ambao mimi binafsi nikiwa ndiye mdhamini nitawezesha fedha shilingi
milioni 13,000,000 ambazo zitasaidia shughuli ya upandaji huu wa miti”,
alisema.
Aliongeza kuwa lengo ni kufikia
idadi ya upandaji miti milioni mbili katika kipindi chake cha miaka sita ya
udhamini wa tamasha hilo, ili iweze kuwanufaisha wananchi hao kufanya biashara
hasa pale watakapofikia hatua ya kupasua mbao na kuuza waweze kupata fedha za
kufanyia maendeleo yao.
Ifikapo mwezi Disemba mwaka
huu uhamasishaji wa upandaji miti hiyo kwa mfumo wa shamba darasa utafanywa pia
katika shule za msingi na sekondari zilizopo kwenye tarafa hiyo ya Namswea kwa
kushirikiana na wananchi ambao wameteuliwa na kwamba kufikia Januari mwaka 2018
vitalu vya kuzalisha miche ya miti vitaanzishwa.
Katika tamasha hilo washindi
mbalimbali wa mchezo wa mpira wa miguu waliweza kuibuka washindi na kujinyakulia
kikombe na fedha taslimu ikiwemo pia na wale walioshiriki michezo ya ngoma za
asili nao waliweza kupewa zawadi na fedha taslimu ambapo kufikia mwakani
michezo zaidi itajumuishwa ikiwemo mbio za baiskeli na mpira wa pete.
Hata hivyo kwa upande wao
wananchi walioshiriki tamasha hilo walipongeza jitihada hizo na kueleza kuwa
wapo tayari kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ikiwemo upandaji
miti ili waweze kunufaika kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.
No comments:
Post a Comment