Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
BAADA ya taarifa ya Kamati maalum iliyofanya kazi ya kuchunguza
uvunaji msitu wa Mbambi uliopo katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani
Ruvuma, kuwasilisha taarifa ya kazi iliyofanya na kubaini hasara ya mapato ya
shilingi milioni 800 ambayo ilibidi yapatikane kutokana na uvunaji huo, baadhi
ya wananchi wamesema kuwa usimamizi wa kazi hiyo ungekuwa mzuri fedha hizo zingepatikana
na kuweza kuboresha huduma muhimu katika hospitali ya wilaya ya Mbinga iliyopo
mjini hapa.
Kadhalika walieleza kuwa hospitali hiyo ambayo hivi sasa
baadhi ya majengo yake ni chakavu likiwemo jengo la upasuaji ambalo halijafanyiwa
ukarabati kwa miaka mingi huku hali ya huduma ikiwa mbaya hivyo wanaiomba
serikali kuchukua hatua ili kuweza kunusuru hali hiyo.
“Hata dawa za kuhudumia akina mama wajawazito pale wanapofikia
hatua ya kujifungua wakati mwingine hazipatikani kwenye hii hospitali yetu na kusababisha baadhi yao
kupoteza maisha lakini fedha hizi zingepatikana zingeweza kuhudumia jamii”, walisema.
Walisema kuwa fedha hizo zingeweza hata kutumika kununua
majokofu ya kuhifadhia maiti katika jengo maalum lililopo katika hospitali hiyo
ya wilaya ambalo limejengwa kwa miaka mingi na halina majokofu hayo huku maiti zikihifadhiwa
katika mazingira magumu.
Hayo yalisemwa na wananchi hao jana kwa nyakati tofauti
wakati walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari huku wakiipongeza Kamati
maalum iliyopewa kazi ya kuchunguza ubadhirifu huo uliojitokeza kwenye uvunaji
wa msitu wa Mbambi uliopo katika kata ya Matarawe mjini hapa.
Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina yao walisema kuwa
baraza maalum la Madiwani ambalo liliketi Oktoba 20 mwaka huu na kupokea
taarifa hiyo limetenda haki kwa wananchi wa Mbinga, kwani wanaimani kuwa ndani
yake itakuwa na ukweli kwa asilimia nyingi hivyo Serikali wameitaka kusimamia
hilo ili mwisho wa siku wahusika wanaotuhumiwa wachukuliwe hatua kali za
kisheria ikiwemo kufikishwa Mahakamani.
Pia walifafanua kuwa kuwepo kwa mikanganyiko ya sahihi katika
mikataba ya uvunaji wa msitu huo na kutofuata sheria ya tangazo la Serikali GN
namba 324 la Agosti 21 mwaka 2015, kuna kila sababu kwa Mkurugenzi mtendaji wa
Halmashauri ya mji wa Mbinga, Robert Kadaso Mageni na watendaji wenzake
wanaotuhumiwa kuhusika katika jambo hili kuchukuliwa hatua ili iweze kuwa
fundisho kwa viongozi wengine wenye tabia kama hiyo.
“Haiwezekani leo hii Rais wetu alimuamini Mkurugenzi huyu na
kumpatia majukumu ya kuongoza halmashauri yetu, halafu hata usimamizi wa mradi
huu wa kuvuna msitu ameshindwa kusimamia kikamilifu badala yake imetokea hasara
ambayo sasa ni aibu na inazorotesha maendeleo yetu”, walisema.
Katika hatua nyingine, kwa mujibu wa nakala ya taarifa ya
uchunguzi wa msitu huo inaeleza pia Kamati maalum iliyofanya kazi hiyo ilibaini
kwamba Afisa misitu wa halmashauri ya mji huo, David Hyera alikuwa anapokea
fedha taslimu kutoka kwa wateja waliokuwa wananunua mbao na baadhi ya fedha
zilikuwa hazipelekwi benki kwenye akaunti husika ya halmashauri.
Kamati hiyo inasema, utaratibu huo uliokuwa ukitumika ulikuwa
unakiuka na kutofuata taratibu za uuzaji wa mali za Serikali ambazo zimeanishwa
kwenye kanuni ya fedha za Serikali za Mitaa (LAFM) mwaka 2009 kifungu namba 45
na kifungu kidogo cha 3 kinachotaka mauzo ya mali za halmashauri zinapaswa
kufanyika kwa njia ya mnada baada ya tangazo la mnada husika kufanyika.
Taarifa hiyo inaongeza pia, Kanuni za Serikali za Mitaa
(Mamlaka za miji) (Maadili ya Madiwani) za mwaka 2000 kifungu cha 28(1)
kinasema; “Pale ambapo afisa wa Serikali za Mitaa kwa makusudi au kwa uzembe
atatoa taarifa za uongo au ushauri mbaya kwa halmashauri na kutokana na taarifa
hizo au ushauri huo unafanywa na kutokana na uamuzi huo halmashauri inaingia
katika hasara, afisa huyo atawajibishwa yeye mwenyewe au kwa pamoja kwa kulipa
hasara iliyopatikana”, inasema sehemu ya taarifa hiyo.
Vilevile uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi
umebaini kuwa kanuni za fedha za Serikali za Mitaa mwaka 2009 kifungu cha 37(2)
kinasema fedha zote zinazokusanywa na wakusanyaji mapato, zinatakiwa
kuwasilishwa kwa mhasibu au benki kabla ya siku ya kazi kwisha au siku ya pili
ya kazi, hivyo basi kama ilikuwa haifanyiki hivyo kuna kila sababu kwa mamlaka
husika kuchukua hatua kwa wahusika wanaotuhumiwa.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya mji wa Mbinga, Mageni
alipohojiwa na waandishi wa habari alisema kuwa yeye hawezi kuzungumzia jambo
lolote hivi sasa juu ya tuhuma hizo za upotevu wa mapato ya uvunaji msitu wa
Mbambi kama zina ukweli au la.
No comments:
Post a Comment