Na Mwandishi wetu,
Songea.
IMEELEZWA kuwa Wajasiriamali wadogo wadogo waliopo katika
halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, watanufaika na mkopo wa
shilingi milioni 49 ambao umetolewa na halmashauri hiyo, kwa ajili ya kuwawezesha
wasonge mbele kimaendeleo katika shughuli zao za ujasiriamali.
Mkuu wa idara ya Maendeleo ya Jamii katika Manispaa hiyo,
Naftari Saiyoloi alitoa taarifa hiyo juzi mjini hapa, katika uzinduzi wa mfuko
wa vijana na wanawake.
Saiyoloi alibainisha kuwa shilingi milioni tisa zitakopeshwa
kwa vikundi kumi vya vijana na shilingi milioni 40 zitakopeshwa vikundi 39 vya
wanawake.
Pia alisema kuwa kuanzia mwaka wa fedha wa 2014/2015 hadi 2017/2018
Manispaa ya Songea imeweza kuwapatia zaidi ya shilingi milioni 181 mfuko wa
wanawake na vijana katika vikundi vyao waweze kufanya shughuli zao za maendeleo.
Kati ya fedha hizo shilingi milioni 116 zinatokana na mapato
ya ndani na zaidi ya milioni 65 zinatokana na marejesho yaliyofanyika kutokana
na vikundi hivyo vinavyokopeshwa kurejesha mkopo husika.
“Idadi ya vikundi vya wanawake vilivyonufaika kwa fedha hizi
ni 202 na kiasi kilichokopeshwa ni zaidi ya milioni 126, idadi ya vikundi 115
vya vijana vilinufaika pia na mkopo wa zaidi ya milioni 55”, alisema Saiyoloi.
Kwa mujibu wa Afisa Maendeleo huyo aliongeza kuwa Manispaa katika
kipindi hicho ilitoa jumla ya shilingi milioni 92 kutoka kwenye mapato yake ya
ndani kwa ajili ya mfuko wa wanawake na vijana.
Alisema kati ya fedha hizo shilingi milioni 3.2 zilitumika
kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji na milioni 88.8 vilikopeshwa vikundi vya
wanawake 77 kiasi cha shilingi milioni 59.8 na vikundi vya vijana 56
vilikopeshwa milioni 29.
Alisisitiza kuwa fedha za vikundi vya wanawake zilizorejeshwa
ni zaidi ya shilingi milioni 53 na fedha za vikundi vya vijana zilizorejeshwa
ni zaidi ya shilingi milioni tisa.
Mgeni rasmi katika utoaji wa mikopo hiyo ambaye alikuwa ni Mbunge
wa Jimbo la Songea mjini, Leonidas Gama alipongeza jitihada hizo zinazofanywa
na Manispaa ya Songea kwa kutoa kwa wakati asilimia kumi ya mapato yake ya
ndani kwa ajili ya kwenda kukopesha vijana na wanawake.
Hata hivyo Gama alisema mikopo hiyo ni muhimu kwa wanawake na
vijana kwa sababu umaskini mkubwa upo katika ngazi ya familia, hivyo itaweza
kupunguza makali ya maisha na hatimaye hata umaskini kupungua kwa wale
waliokuwa wanyonge.
No comments:
Post a Comment