Hii ni moja kati ya sehemu ya barabara mtaa wa FFU kwenda Matogoro yenye urefu wa kilometa 3.2 inayojengwa kwa kiwango cha lami nzito katika Manispaa ya Songea. |
Na Mwandishi wetu,
Songea
HATIMAYE Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,
imevunja rasmi Mkataba ujenzi wa lami nzito kati yake na Kampuni ya Lukolo
yenye makao makuu yake Jijini Dar es salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa hiyo, Mhandisi
Samwel Sanya alisema kuwa wamechukua maamuzi hayo baada ya muda wa Mkataba wa
kumaliza kazi kwa Mkandarasi huyo ulimalizika tangu Juni 30 mwaka huu.
Alisema kuwa baada ya muda huo kumalizika Mkandarasi huyo
aliingizwa kwenye tozo (Liquidated Damage) na kwamba iwapo atashindwa kumaliza
kazi kwa siku 100 hatua za kisheria za kuvunja mkataba zitafanyika.
“Oktoba 8 mwaka huu ndiyo siku 100 alizopewa Mkandarasi huyo
zimemalizika hivyo tumevunja mkataba rasmi na Mkandarasi huyu, amekatwa
asilimia 10 ambayo ni sawa na shilingi bilioni 1.4 kwa kuchelewesha mradi na anatakiwa
kulipa asilimia 15 ya fedha kwa kazi ambazo hajamaliza ndani ya mkataba”,
alisema Sanya.
Mkandarasi huyo pia anatakiwa kurudisha kiasi cha fedha shilingi
bilioni 2.15 ambazo zilitolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) fedha
ambazo zilitolewa kwa ajili ya kufanya kazi ya kusafirishia mitambo mbalimbali
ya ujenzi katika mradi huo.
Kaimu Mkurugenzi huyo wa Manispaa ya Songea alifafanua kuwa baada
ya kuvunjwa mkataba huo, Manispaa itaanza mchakato wa kumtafuta Mkandarasi
mwingine ili aweze kuendelea na kazi zilizobaki katika ujenzi wa barabara hiyo.
Zaidi ya shilingi bilioni 14 zinatarajiwa kutumika katika
ujenzi wa barabara za mji wa Songea katika kiwango cha lami nzito zenye urefu
wa kilometa 8.6.
Fedha za mradi huo zimetolewa na Benki ya Dunia chini ya Mpango
wa kuzijengea uwezo Serikali za mitaa (ULGSP), ambapo mpango huo unakusudia
kuendeleza miundombinu ya Halmashauri za Miji na Manispaa 18 za Tanzania bara
ikiwemo Manispaa hiyo.
Mradi huo ambao ulianza kujengwa Juni Mosi mwaka 2015
ulitarajiwa kukamilika Juni 30 mwaka huu ambapo fedha iliyopokelewa na Manispaa
ni zaidi ya shilingi bilioni saba ambapo
hadi sasa Mkandarasi huyo alikwisha lipwa zaidi ya shilingi bilioni nne.
Barabara za Manispaa ya Songea ambazo zipo kwenye mradi huo ni
katika mtaa wa FFU hadi Matogoro yenye urefu wa kilometa 3.2, barabara ya shule
ya sekondari ya wasichana Songea hadi Mateka yenye urefu wa kilometa 1.5 na barabara
ya Mwembechai hadi Bombambili yenye urefu wa kilometa 2.6.
Vilevile barabara nyingine ni Mitumbani hadi Yapenda yenye
urefu wa kilometa moja, barabara ya Polisi hadi Stendi ya Mlilayoyo yenye urefu
wa kilometa 0.45.
No comments:
Post a Comment