Baadhi ya wananchi waliopo kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini katika Manispaa ya Songea wakipata huduma. |
Na Albano Midelo,
Songea.
MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Halmashauri ya
Manispaa ya Songea mkoani Euvuma, imeweza kuwasaidia wanufaika 4,881 waliopo kwenye
mpango wa kunusuru kaya maskini katika halmashauri hiyo kwa kuwapatia shilingi
milioni 175 ili ziweze kuwasaidia na hatimaye waweze kuondokana na umaskini.
Christopher Ngonyani ambaye ni Mratibu wa mfuko huo katika
halmashauri hiyo alimweleza mwandishi wetu kuwa fedha hizo zimetolewa katika
kipindi cha mwezi Septemba hadi Oktoba mwaka huu.
Alisema malipo hayo yamefanyika na kukamilika ndani ya wiki
hii katika mitaa 53 ambayo ina wanufaika hao.
Ngonyani alibainisha kuwa kati ya fedha hizo zaidi ya shilingi
milioni 133 wamelipwa wanufaika 3,608 kwa njia ya fedha taslimu na shilingi
zaidi ya milioni 42 wamelipwa wanufaika 1,273 kwa njia ya mitandao ya simu.
Alisema malengo waliyojiwekea ni kuhakikisha kwamba wanufaika
wote wa TASAF wanaingizwa kwenye mfumo wa malipo kwa njia ya mtandao huo kwa
kuwa malipo yamekuwa yakilipwa moja kwa moja na TASAF kutoka makao makuu Dar es
Salaam, badala ya fedha kutumwa katika halmashauri kitendo ambacho hutumia muda
mrefu hadi kuwafikia walengwa.
Utafiti uliofanywa katika mitaa mbalimbali ambayo wanufaika hao
wamelipwa kwa njia ya mtandao, umebaini kuwa mfumo huo umepata mafanikio
makubwa baada ya wanufaika wengi kupata fedha zao kwa wakati, ingawa changamoto
ilijitokeza kwa baadhi ya kampuni za simu kushindwa kuwalipa wanufaika kwa njia
ya mtandao.
Manispaa ya Songea ni moja kati ya halmashauri 16 nchini
zilizochaguliwa kufanya majaribio ya malipo kwa njia ya mtandao wa simu kwa
wanufaika wa TASAF ili kuepukana na changamoto zilizokuwa zimejitokeza za kutumia mfumo wa kulipwa fedha taslimu.
Hata hivyo mpango wa kunusuru kaya maskini hapa nchini
umekuwa ukiendeshwa katika halmashauri 163 na kwamba mpango huo umezinufaisha
kaya maskini zikiwemo zile ambazo awali zilikuwa zinapata mlo mmoja kwa siku
ambapo hivi sasa wanaweza kupata milo mitatu kwa siku.
No comments:
Post a Comment