Na Mwandishi wetu,
Dodoma.
MTU mmoja amefariki dunia na wengine nane kuugua ugonjwa wa
kipindupindu mkoani Dodoma, ambapo inadaiwa kuwa ugonjwa huo uliwapata wakiwa
kwenye sherehe ya harusi iliyofanyika katika kijiji cha Mlowa barabarani
wilayani Chamwino.
Dokta Charles Kiologwe ambaye ni Mganga mkuu wa Mkoa wa
Dodoma alisema kuwa ugonjwa huo uliingia mkoani humo Oktoba 19 mwaka huu huku akizitaja
wilaya zilizokumbwa na ugonjwa kuwa ni Bahi, Chamwino na Kongwa.
Alisema ugonjwa wa kipindupindu umeingia katika mkoa wa
Dodoma ambapo baadhi ya watu wameugua na mmoja amepoteza maisha wilayani Bahi.
Dokta Kiologwe alisema ugonjwa huo uliibuka kwenye sherehe hizo
ambako kulikuwa na mkusanyiko mkubwa wa watu kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa
huo na kwamba baada ya sherehe hizo kumalizika, siku ya pili watu wawili wa
familia moja waligundulika kuugua ugonjwa huo.
Alisema kuwa timu ya madaktari wa mkoa kwa kushirikiana na wa
wilaya ya Chamwino walifungua kambi ya muda ili kuweza kuzuia hali hiyo isiweze
kuenea.
“Baada ya kudhibiti ugonjwa huu kwenye wilaya ya Chamwino tulipata
taarifa ya mgonjwa mwingine ambaye alikuwapo kwenye sherehe hiyo ambaye ni mkazi
wa Chibelela wilayani Bahi kuwa anaugua ugonjwa huu tumeweza kuchukua hatua na
kudhibiti hali hii”, alisema Dokta Kiologwe.
Alibainisha kuwa mume wa mgonjwa huyo wakati akimuuguza mke
wake huyo hakujua kama ana ugonjwa wa kipindupindu kwa kuwa alikuwa akimuuguza
kienyeji na matokeo yake na yeye akakumbwa na kipindupindu na kumsababishia
kifo.
Vilevile alisema wagonjwa wengine wawili waliokuwa safarini
wakitokea kijiji cha Mlowa barabarani waliugua ugonjwa huo na kulazimika
kulazwa katika Kijiji cha Nkurabi ili kupatiwa matibabu.
Dokta Kiologwe alieleza kuwa mpaka sasa watu tisa wameugua
ugonjwa huo na kati yao mmoja amefariki na tayari hatua zimechukuliwa kwa
kufungua kambi za muda kijiji cha Mlowa barabarani (Chamwino), Chibelela
(Bahi), Nkurabi (Manispaa ya Dodoma) na Kongwa.
Alitoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari za ugonjwa huo
kwa kufanya usafi na kuzingatia kanuni za afya katika maeneo yao wanayoishi ili
kuweza kujiepusha na kukumbwa na ugonjwa huo.
No comments:
Post a Comment