Na Albano Midelo,
Songea.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imeanza
rasmi upuliziaji wa dawa kwa ajili ya kuua mazalia ya Mbu katika mitaa iliyopo
kwenye kata 21 zilizopo ndani ya Manispaa hiyo.
Afisa afya wa Manispaa ya Songea, Vitalis Mkomela alisema kuwa
zoezi la upuliziaji lilianza Oktoba 19 mwaka huu katika mitaa ya kata za
Bombambili, Mfaranyaki, Matarawe na Mjini.
Mkomela alifafanua kuwa zoezi hilo limefanyika katika maeneo
yenye mazalia ya mbu ambayo ni ya wazi yenye kuzalisha mbu wanaotaga mayai na kueneza
ugonjwa wa malaria.
Kwa mujibu wa Afisa afya huyo hadi sasa jumla ya mazalia ya
maji 212 na mabwawa nane yamepuliziwa dawa na kwamba zoezi hilo ni endelevu litafanyika
kata hadi kata.
Amezitaja changamoto ambazo zimejitokeza hadi sasa ni kwamba utekelezaji
wake umekuwa mgumu kutokana na kukosa fedha za kununua vifaa na kuwalipa wapuliziaji.
Kufuatia hali hiyo wameweza kuanza katika mitaa 49 tu iliyopo
katika kata kumi kati ya mitaa 95 iliyopo katika kata 21 ndani ya Manispaa hiyo.
Changamoto nyingine ni kukosekana kwa maafisa afya katika
kata nane ambao ni wataalam ambao wangeweza kusaidia katika utekelezaji wa kazi
hiyo.
Pamoja na mambo mengine Afisa afya huyo anaongeza kuwa mikakati
ambayo inachukuliwa ili kuweza kukabiliana na changamoto hizo kuwa ni kuandaa
bajeti ya upuliziaji na kuiingiza katika mpango wa utekelezaji wa mwaka 2018/2019
ili kuweza kuleta ufanisi zaidi.
Kabla ya kuanza rasmi kwa zoezi la upuliziaji Manispaa ya
Songea ilianza kutekeleza kazi hiyo kwa kuwashirikisha viongozi wa mitaa kwa
kufanya nao mikutano elekezi wakiwemo Wenyeviti na Maafisa watendaji.
Mikutano hiyo walikuwa wakijadili masuala muhimu juu ya namna
zoezi la kuua viluwiluwi vya mbu, kuhamasisha wananchi katika kutambua mazalia
ya mbu na namna ya kukabiliana nayo katika maeneo yao huku wakimteua pia mpuliziaji
wa viuadudu ambaye atajitolea katika kufanya kazi hiyo.
Mkomela alisema baada ya mkutano huo Wenyeviti wa mitaa na Maafisa
watendaji waliweza kuteua mpuliziaji kutoka katika kila mtaa ambao walipewa
mafunzo namna ya kupulizia viuadudu katika maeneo ambayo yana mazalia wazi na yale
yaliyofunikwa.
No comments:
Post a Comment