Sunday, November 5, 2017

MAKALA: MWAKA 1922 WATANGANYIKA WALINYIMWA VYEO KATIKA MAJESHI YA ULINZI

Na  Kassian Nyandindi,

USALAMA wa jumuiya ama jamii ni jambo la msingi katika kusongesha mbele gurudumu la maendeleo siku zote za maisha ya binadamu.

Hatua ya kuhitaji usalama kwa kila binadamu ni kutokana na kuzungukwa na makundi mbalimbali ya waasi ambao kwa tafsri ya haraka, tafiti zinawabainisha kama wasaliti wakuu katika maisha.

Madhara makubwa yanayosababishwa na waasi hao ama wahalifu kwa jina lingine ni kufanya mashambulizi ambayo huchangia hata idadi kubwa ya watu kupoteza maisha achilia mbali upotevu wa mali.


Kutokana na familia nyingi kukabiliwa na vikwazo vya kushambuliwa na matatizo mbalimbali na hata kupoteza ndugu na jamaa.

Tokea nchi hii ipate Uhuru kutokana mashambulizi hayo ya wahalifu sote tufarijiane kwa pamoja na tuendelee kudumisha usalama na amani katika maeneo yanayotuzunguka.

Kadhalika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambayo iliundwa Desemba 15 mwaka 1961 baada ya Tanganyika kupata Uhuru ilikuwa na dhamira njema ya kuwahakikishia Watanzania usalama wao na mali zao.

Kuanzishwa kwa Wizara hiyo tafiti zinaonesha kuwa ililenga kuunda chombo ambacho kingesimamia masuala ya ulinzi na usalama wa raia na mali zao katika mazingira ya nchi huru.

Ili kuiwezesha nchi yetu kuondokana na sera za kikoloni ambazo zilianzishwa kwa ajili ya kulinda maslahi ya wakoloni. 

Majukumu ya Wizara hii yalitekelezwa kwa kupitia Jeshi la Polisi na idara ya magereza wakati ambao utawala wa Kijerumani haukuanzisha jeshi rasmi la polisi badala yake walikuwa wakiwatumia watawala wa vijiji wakiwemo Maakida na Majumbe katika kutekeleza majukumu ya kipolisi.

Kwa upande mwingine askari wa jeshi na vikundi vingine vya ulinzi ambao walijulikana kitaalam kama Para–military groups vilitumika kudhibiti upinzani wa ndani pamoja na kulinda mipaka.

Mwaka 1916 Wajerumani walianzisha Jeshi la Polisi la kiraia kitaalam lilikuwa likiitwa Civilian Police Force baada ya kuelekea kushindwa na majeshi ya Kiingereza katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia tangu mwaka 1910 kwa lengo la kulinda vitega uchumi, makazi yao na mipaka ya koloni la Tanganyika.

Kikosi hicho cha Polisi kilichokuwa na askari 31 chini ya Meja Davies kutoka Afrika ya Kusini, kilitekeleza majukumu ya kipolisi hadi mwaka 1919 Wajerumani waliposhindwa na Waingereza.

Wakati wa utawala wa Waingereza tafiti zinaeleza kwamba walianzisha taasisi mbalimbali ikiwemo Jeshi la Polisi lilojulikana kama Tanganyika Police Force and Prisons Service chini ya Sheria ya Jeshi la Polisi na Magereza ya mwaka 1919 yaani The Police Force and Prisons Ordinance Cap.40.

Agosti 25 mwaka 1919 Serikali ya Kiingereza ilianzisha rasmi Jeshi la Polisi kupitia tangazo la gazeti la Serikali namba 1.Vol.I No. 21-2583 hatua ambayo ilisababisha makao makuu ya jeshi la polisi kuwa Lushoto eneo la Wilemstal mjini Tanga.

Kwa mujibu wa kumbukumbu zinaeleza kuwa, Meja Davies aliteuliwa kuwa Kamishna wa kwanza wa Jeshi hilo na baadaye nafasi yake ilichukuliwa na Meja Brownie Esq aliyehamishwa kutoka Kenya.

Tofauti na utawala wa Kijerumani, jeshi hilo lilipewa majukumu ya kipolisi, magereza, usalama wa taifa, kimahakama na ya kiutawala pale ambapo hapakuwa na maofisa tawala au wakuu wa wilaya.

Ingawa Jeshi la Polisi lilijitenga na shughuli za kijeshi bado lilikuwa na jukumu la kulinda maslahi ya wakoloni wa Kiingereza.

Hali hii ilijionesha kwenye muundo wa Jeshi la Polisi ambapo nafasi za juu zilishikwa na wazungu, nafasi za kati zilishikwa na Waasia na vyeo vya chini vilibaki kwa wazawa.

Mwaka 1922 kulikuwa na wazungu 68 wenye vyeo kuanzia wakaguzi hadi makamishna ambapo wakaguzi 25 wenye asili ya Asia na Waafrika 748 wa vyeo vya chini.

Pamoja na kuongezeka kwa idadi ya Waafrika ndani ya jeshi la polisi, hali ya kubaguliwa iliendelea huku tafiti zikitolea mfano mwaka 1930  jeshi hili lilikuwa na Wazungu 78 kwenye nafasi za juu, Waasia 67 kwenye vyeo vya kati na Waafrika 1719 kwenye nafasi za chini.

Mbali na kushika nafasi za chini katika jeshi hilo, Waafrika pia walibaguliwa kwa taratibu za kiutawala, makazi na stahili.

Wakati wa Utawala wa Kiingereza shughuli za kipolisi zilifanywa kwenye maeneo ya miji na vijiji vilivyokuwa na idadi kubwa ya walowezi wa kizungu.

Katika maeneo haya vituo vya polisi vya muda yaani Detached Police Stations vilianzishwa kwa ajili ya kulinda mashamba ya walowezi.

Katika kipindi cha Vita Kuu ya Pili ya Dunia ambayo ilichukua hatamu tangu mwaka 1939 hadi 1945 utawala wa Kiingereza ulipanua wigo wa ajira ndani ya jeshi la polisi na kuongeza idadi ya Maofisa wa Kiafrika katika nafasi za kati na za juu.

Tafiti zinabainisha kuwa kufikia mwaka 1960, kulikuwa na Waafrika 28 kwenye ngazi za juu za Jeshi la Polisi.

Kwa upande wa Zanzibar jeshi la polisi lilianzishwa mwaka 1873 kwa ajili ya kusimamia sheria za kupinga biashara ya utumwa.

Jeshi hili lilijumuisha askari wa Kiingereza na wa Sultani wa Zanzibar.

Mwaka 1877 Serikali ya Kiingereza ilimteua Kamanda wa Kikosi cha Maji, Lloyd Mathews, kuongoza askari 1300 wakiwemo Waafrika 300.

Mwaka 1907 wakati Zanzibar ikiwa chini ya uangalizi wa Waingereza kitaalam Protectorate, Sultani alilivunja jeshi la polisi baada ya askari wake kugoma kutokana na mishahara midogo na mazingira duni ya kazi na kuunda lingine ambalo lilijumuisha askari wa akiba kutoka Tanganyika.

Baada ya Tanganyika kupata uhuru wake Desemba 9, 1961 jukumu la Jeshi la Polisi lilibadilika kutoka kusimamia maslahi ya kikoloni na kuwa jeshi la kusimamia utekelezaji wa sheria ndani ya Tanganyika huru.


Hivyo basi, kimsingi muundo na majukumu ya Jeshi la polisi yalibaki kama yalivyo igawa mabadiliko makubwa yaliyojitokeza wakati huo ni kuongezeka kwa Maofisa wa Kiafrika wenye vyeo vya juu ili kuchukua nafasi zilizokuwa zikishikiliwa na Wazungu.

No comments: