Saturday, November 25, 2017

MIGOGORO NAMTUMBO YAMCHUKIZA WAZIRI MKUU ASEMA INAKWAMISHA KUKUA KWA MAENDELEO YA WANANCHI

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa.
Na Kassian Nyandindi,    
Namtumbo.

SERIKALI imewataka watumishi wa umma wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, kuchapa kazi na kujiepusha kufanya kazi kwa mazoea ili waweze kuleta tija sehemu ya kazi badala ya kutumia muda mwingi katika migogoro inayorudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipokuwa akizungumza na watumishi wa umma wa wilaya hiyo akiwa katika siku yake ya kwanza ya ziara ya kikazi siku tatu mkoani Ruvuma.

Alisema kuwa Serikali imedhamiria kuwatumikia na kuwaletea maisha bora wananchi, hivyo kila mtumishi ni lazima awajibike kwa kufanya kazi ipasavyo kwa lengo la kuchochea kukua kwa haraka maendeleo ya wilaya na wananchi wake kwa ujumla.

Alisema Serikali inayoongozwa na Dokta John Pombe Magufuli imedhamiria kuboresha maisha ya wananchi na kazi hiyo itafanywa na watumishi wa umma kwa hiyo hakuna muda wa kumbembeleza mtumishi ambaye atakwamisha mikakati ya kuharakisha maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi.

Vilevile amewaagiza watumishi wote wa halmashauri ya wilaya ya Namtumbo kushirikiana na Madiwani wao katika kazi zao za kila siku ili kwa pamoja waweze kumaliza kero za wananchi ambao wanasubiri kufaidi matunda ya Serikali yao ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu huyo amewataka Madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo kutumia vikao vyao halali kupanga mikakati inayolenga kuibua vyanzo vya mapato, badala ya kuwa sehemu ya kundi la walalamikaji ambao wanasubiri kuona viongozi wa juu wanakwenda kumaliza matatizo yao na ya wananchi wanaowaongoza.

Majaliwa aliwaonya viongozi wa wilaya kuhakikisha wanamaliza migogoro ya muda mrefu ambayo ipo wilayani humo inayosababisha kukwamisha juhudi za kuleta maendeleo na kuharakisha kukua kwa uchumi.

“Mkuu wa wilaya tumekuleta hapa Namtumbo ili uwe kiungo muhimu kati ya watumishi, madiwani na wananchi, haiwezekani kila siku ninyi ni sehemu ya watu wa migogoro tu isiyokwish”, alisema.

Awali Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Christine Mndeme alisema kuwa wilaya hiyo ina upungufu wa watumishi 1,298 kati ya watumishi 3,175 wanaohitajika na kwamba waliopo sasa ni watumishi 1,877.

Licha ya upungufu huo Serikali bado itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kuwatumikia wananchi kwani inaamini changamoto hiyo na nyingine zitaendelea kushughulikiwa kadri fedha zitakapopatikana.

No comments: