Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida,
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, Robert
Kadaso Mageni amezungumza katika baraza la Madiwani wa halmashauri ya mji huo akieleza
kwamba matatizo yaliyojitokeza nyuma kati yake na Madiwani hao hakuna ubaya
wowote na kazi zinaendelea kufanyika.
Mageni alisema hayo juzi mbele ya
msaidizi wa Katibu tawala wa mkoa huo, Joel Mbewa katika kikao cha Madiwani
kilichoketi kwenye ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi mjini hapa.
Madiwani hao walipozungumza kwa
nyakati tofauti na mwandishi wetu walisema kuwa kufuatia mgogoro mzito
unaoendelea kufukuta kati yake na Madiwani wa mji huo, juu ya uvunaji wa msitu
wa Mbambi ambao anashutumiwa kwamba yeye na baadhi ya watendaji wake wametafuna
kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 800 ndiyo maneno hayo sasa amekuwa
akiyazungumza kwa lengo la kutaka kujisafisha.
Walisema kauli hiyo ya Mkurugenzi
huyo inafuatia pia Madiwani hao katika kikao walichoketi Oktoba 27 mwaka huu
kumkataa hawataki kufanya naye kazi tena.
Vilevile sakata hilo la kumkataa
liliwafanya wasipokee agenda za kikao na hatimaye wote walitoka nje ya kikao na
kuacha kuendelea nacho ndipo juzi Novemba 14 mwaka huu, baada ya taratibu
husika kufanyika na kupitia vikao mbalimbali wameweza Madiwani hao kukutana kwa
pamoja na kujadili tena agenda za maendeleo ya wananchi na sio mgogoro wa msitu
huo ambao unasubiri maamuzi yake baada ya kufikishwa ngazi za juu Serikalini.
Pamoja na mambo mengine, Mageni
alionekana kutumia muda wake kwa mtindo wa “kujisafisa” akisema yeye anatambua
kwamba baraza hilo la Madiwani wanapaswa kusafiri meli moja katika wajibu wa
kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote
yaliyotokea matokeo yapatikane suala la mtikisiko wa pamoja lakini safari yetu
ni lazima tuwatumikie wananchi, kama mnavyofahamu Mheshimiwa Rais John Pombe
Magufuli ametuamini tutekeleze maendeleo ya wananchi,
“Hakuna ubaya wowote kazi tunaendelea
kufanya kama tulivyokuwa tunafanya kuhakikisha Serikali yetu tunafikisha lengo
katika kusukuma mbele maendeleo”, alisema Mageni.
Kadhalika alimuomba Mwenyekiti wa
halmashauri ya mji wa Mbinga, Kipwele Ndunguru pamoja na Madiwani wake waendelee
kushirikiana kutekeleza maendeleo ya wananchi.
Awali akizungumza katika baraza hilo,
msaidizi wa Katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma, Joel Mbewa alisema kuwa kuanzia
sasa viongozi wa kutoka ngazi ya mkoa Ofisi ya Katibu tawala watakuwa
wanahudhuria kikao hicho cha baraza la Madiwani kila kitapokuwa kinafanyika.
“Madiwani niwasisitize mnapokuwa
kwenye vikao vyenu vya CMT muwe mnajenga hoja na misimamo yenu huko kwa kutoa
mawazo yenu na matatizo yaliyopo kwenye kata ili yaweze kufanyiwa kazi”,
alisema Mbewa.
Pia amewataka washirikiane na Mkaguzi
wa ndani pamoja na Mwanasheria wa halmashauri katika kusimamia miradi
mbalimbali ambayo inatekelezwa ndani ya halmashauri.
“Mwanasheria na Mkaguzi wa ndani haya
ndiyo macho mawili ndani ya halmashauri yenu ambayo yanatusaidia katika kuona
mbali zaidi tushirikiane nao kutatua matatizo”, alisisitiza.
Mbewa alieleza kuwa halmashauri pia
inatakiwa kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa mapato ili utekelezaji wa miradi
ya wananchi uweze kufanyika ipasavyo.
No comments:
Post a Comment