Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
HATIMAYE Wananchi wa kata ya Lusonga
waliopo katika halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, wamerejeshewa
viwanja vyao ambavyo vilitwaliwa kwa muda mrefu na halmashauri hiyo kwa
makubaliano kwamba watalipwa fidia.
Muafaka wa kurejesha viwanja mikononi
mwa wananchi wa kata hiyo ulifikia juzi kwenye kikao cha baraza la Madiwani wa
mji huo, lilikoketi kwenye ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi uliopo
mjini hapa.
Hatua hiyo imefikia baada ya Madiwani
hao kulalamikia hali hiyo kwa muda mrefu bila kufanyiwa utekelezaji, huku
baadhi ya wananchi walianza kuvamia viwanja hivyo na kufanya shughuli zao
binafsi kutokana na halmashauri kushindwa kuwalipa fedha zao kwa mujibu wa
makubaliano yaliyofanyika hapo awali.
“Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,
Dokta Binilith Mahenge aliagiza kwamba kama halmashauri haina fedha ya kuwalipa
wananchi wale kwa wakati, yale maeneo yarudishwe mikononi mwa wananchi”,
alisema diwani wa kata ya Matarawe Leonard Mshunju.
Naye diwani wa kata ya Kitanda Zeno
Mbunda aliongeza kuwa ni jambo la busara limefanyika kujadili tatizo hilo mbele
ya baraza la Madiwani kwani wananchi wa kata ya Lusonga walifikia katika hatua
ambayo sio nzuri kwa lengo la kutaka warejeshewe viwanja vyao.
Hata hivyo hatimaye baraza hilo
kupitia Mwenyekiti wake, Kipwele Ndunguru walifikia muafaka kwamba wananchi hao
wakabidhiwe viwanja vyao haraka kwa kufuata taratibu husika kutokana na
halmashauri hiyo hivi sasa haina fedha za kuweza kuwalipa fidia.
No comments:
Post a Comment