Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Christine Mndeme amesema kuwa
mtumishi yeyote ambaye amekuwa na mazoea ya kufanya kazi kwa mfumo wa ufisadi,
majungu na fitina katika utawala wake mkoani humo hana nafasi tena badala yake atafute
sehemu nyingine ya kwenda kufanyia kazi.
Kadhalika amewataka watumishi hao wasifanye kazi kwa mazoea
bali wanapaswa kuwa wazalendo zaidi katika kazi, ikiwemo kuonesha uhalali wao wa
kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais Dokta John Pombe Magufuli katika
kutekeleza shughuli za maendeleo ya wananchi.
Mndeme alisema hayo juzi wakati alipokuwa katika ziara yake
ya kikazi wilayani humo, akizungumza na baadhi ya watumishi wa Serikali wa kada
mbalimbali pamoja na Madiwani mjini hapa.
“Kila mtu katika kazi yake ajitambue kuwa ni muhimu katika
jamii, ndugu zangu wafanyakazi wa Mbinga ninachowataka kuwaambia hapa ondokeni
na kufanya kazi kwa mazoea”, alisisitiza.
Alisema kuwa hapendi kuona matumizi ya fedha za Serikali
yanakwenda ovyo hivyo amewataka watumie fedha vizuri kwa kufuata miongozo
iliyowekwa katika shughuli yenye tija kwa ajili ya kuwaletea maendeleo
wananchi.
Mkuu huyo wa mkoa alibainisha kuwa semina na posho kwa safari
ambazo hazina umuhimu hataki kusikia badala yake wanapaswa kubana matumizi.
“Viongozi mliopewa dhamana acheni kukaa maofisini muda mwingi
utumieni kuwa karibu na wananchi kule vijijini kusikiliza kero zao na
kuzitekeleza kwa wakati”, alisema Mndeme.
Vilevile aliwashutumu maafisa utumishi kuwa mara nyingi
wamekuwa hawaendi vijijini kuonana na viongozi wa ngazi ya vijiji na kata
katika kutatua matatizo mbalimbali, badala yake hivi sasa amewataka waende huko
kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Pamoja na mambo mengine, alikemea pia tabia ya uchomaji moto misitu
huku akiwataka maafisa misitu ambao ndiyo wamepewa dhamana ya kusimamia hilo
wahakikishe wanazuia shughuli za uharibifu wa mazingira, ikiwemo katika vyanzo
vya maji ambapo alisisitiza wasiwe na huruma pale wanapomkamata mtuhumiwa
haraka wamfikishe kwenye vyombo vya kisheria ikiwemo Mahakamani.
No comments:
Post a Comment